Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Wagombea wenza walivyokwepa mdahalo na kuwaibisha Wakenya

Wakenya wamekasirishwa na hatua ya wagombea wenza saba akiwemo Naibu rais William Ruto na Kalonzo Musyoka kutoka muungano mkuu wa upinzani NASA kutojitokeza kushiriki katika mdahalo wa runinga siku ya Jumatatu usiku.

Mgombea mwenza pekee aliyejitokeza katika mdahalo wa urais nchini Kenya  Eliud Muthiora Kariara Julai 17 2017
Mgombea mwenza pekee aliyejitokeza katika mdahalo wa urais nchini Kenya Eliud Muthiora Kariara Julai 17 2017 DebatesKE
Matangazo ya kibiashara

Waandalizi wa mdahalo huo ambao ni wamiliki wa vyombo vya Habari nchini Kenya, wamejitokeza na kusema wagombea wenza wote walishirikishwa mapema kuhusu mdahalo huo, na ni aibu kutojitokeza kueleza mipango yao kwa wananchi wa taifa hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu tarehe nane mwezi ujao.

Ruto amedai kuwa alifahamu mdahalo huo kupitia vyombo vya Habari huku Kalonzo akisema kuwa hakuwa tayari kwenda katika mdahalo huo bila ya uwepo wa Ruto ambaye ni Naibu rais.

Wagombea wenza wengine sita waliokuwa wamepangiwa kushiriki katika mdahalo huo kuanzia saa 11 na nusu jioni walionekana kutoridhishwa na muda waliopangiwa na kuamua kuwasili wakati wa mdahalo wa pili lakini wakazuiwa.

Ruto na Kalonzo walitarajiwa kuanza mdahalo wao kuanzia saa mbili na nusu usiku. Mfumo huo ulifikiwa kutokana na umaarufu wa wagombea wenza hao kwa mujibu wa tafiti za kura ya maoni nchini humo.

Wakenya walio wengi wanasema hatua hii ni dharau na wanasiasa wameonesha hofu ya kutokuwa tayari kuwajibikia masuala muhimu ya taifa ambayo walitakiwa kuyatolea ufafanuzi kama uchumi, ufisadi na uongozi bora.

Mchambuzi wa siasa na mgombea binafsi wa Ugavana wa Kaunti ya Nairobi Miguna Miguna, amesema kitendo cha wanasiasa hao ni cha aibu na wameonesha wazi kuwa hawako tayari kuhojiwa na wananchi.

Miguna amewafananisha wagombea wenza hao kama watu wanaomba kazi lakini wamekataa kwenda kufanyiwa usaili ili kumpata mfanyikazi bora.

Hata hivyo, Eliud Muthiora Kariara mgombea mwenza binafsi alionesha ushupavu wa kipekee na kujitokeza katika mdahalo huo na kupata muda wa dakika 90 kujieleza na kuwapa nafasi Wakenya kumfahamu zaidi.

Licha ya uchanga wake kisiasa, Kariara ambaye ni kijana alionesha ukakamavu na kujitahidi kujieleza kwa ufasaha kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili na kuahidi mabadiliko ya kiuchumi na pia kuunda nafasi za ajira ikiwa watashinda Uchaguzi Mkuu.

Kujitokeza kwake, kumepongezwa na wakenya, wachambuzi wa siasa na waandalizi wa mdahalo huo ambao wamesema atakuwa mwanasisa shupavu siku zijazo.

Raphael Tuju, Katibu Mkuu wa chama tawala Jubilee licha ya kukiri kuwa kulikuwa na mawasiliano ya karibu  na waandaji wa mdahalo huo, ameeleza kuwa sababu kubwa iliyosababisha mgombea mwenza wa chama chake kutofika ni kutokana na tofauti mbaimbali zilizovuka dakika za lala salma.

Jubilee walitaka kumfahamu atakayeongoza mdahalo huo, masuala yatakayojadiliwa lakini pia wale wataokaohudhuria mdahalo huo na kuuliza maswali.

Salim Lone msemaji wa mgombea urais Raila Odinga, kwa upande wake amesema kwa upande wao kama NASA, hawakuwa na tatizo la kujitokeza katika mdahalo huo lakini walichohitaji ni kujitokeza kwa wapinzani wao wa karibu wa Jubilee.

Wakenya hata hivyo, wanaendelea kuwa na imani kuwa mdahalo wa wagombea urais uliopangwa kufanyika Jumatatu ijayo utahudhuriwa na wagombea wote akiwemo rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

Wadadisi wa siasa wanaona kuwa kwa kiasi fulani midahalo hii huenda ikabadilisha mawazo ya wapiga kura nchini humo.

Vyombo vya Habari nchini Kenya vinasema vimetekeleza jukumu lao kwa wananchi ya Kenya kwa kutoa fursa hiyo  kama walivyoahidi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.