Pata taarifa kuu
KENYA- UCHAGUZI 2017

Fahamu ahadi zinazotolewa na wagombea urais nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu

Kampeni zinaendelea kwa mwezi wa pili nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini humo tarehe nane, mwezi Agosti mwaka huu.

Wagombea urais nchini Kenya Uhuru Kenyatta na  Raila Odinga
Wagombea urais nchini Kenya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga DR.
Matangazo ya kibiashara

Wadhifa wa urais umewavutia wagombea wanane ambao ni pamoja na rais Uhuru Kenyatta, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga anayewania wadhifa huo kupitia muungano wa vyama vya  upinzani NASA na Cyrus Jirongo kupitia United Democratic Party (UDP).

Wengine ni pamoja na Ekuru Aukot  wa Thirdway Alliance, Abduba Dida kutoka chama cha Alliance for Real Change (ARC), na wagombea binafsi Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japheth Kavinga.

Licha ya uchaguzi huu kuwa na wagombea wengi, ushindani ni kati ya rais Uhuru Kenyatta anayewania kwa muhula wa pili na Raila Odinga anayetafuta urais kwa mara ya nne sasa.

Ahadi za chama tawala.

Rais Uhuru Kenyatta anaendelea kuahidi kuwa ikiwa itachaguliwa tena, mradi wa Wakenya wengi kupata nguvu za umeme utaendelea.

Aidha, anajivunia kumalizika kwa reli ya sasa na kuzindua safari za treni kutoka Mombasa hadi jiji kuu la Nairobi.

Rais Kenyatta amekuwa akisema, kipindi cha miaka minne iliyopita, serikali yake imefanikiwa kujenga barabara mpya za lami zinazokadiriwa kuwa na urefu wa  Kilomita 10,000. Hata hivyo, upinzani umekuwa ukisema huu ni uongo.

Kuhusu Elimu, Kenyatta na chama cha Jubille anaahidi kuwa kuanzia mwaka ujao, elimu itakuwa bure katika shule zote za serikali kutoka kidato cha kwanza hadi kile cha nne.

Ahadi za NASA

Mgombea wa upinzani Raila Odinga, anaahidi kuwa ikiwa serikali ya NASA itaingia madarakani, katiba ya nchi hiyo itatekelezwa ipasavyo na kuhakikisha kuwa serikali ya Kaunti zinafanya majukumu yao ipasavyo.

NASA inaahidi kuwa, elimu katika shule za sekondari kutoka kidato cha kwanza hadi cha nne  itakuwa bure kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.

Upinzani umekuwa ukisema kuwa serikali ya Jubilee, imeshindwa kuonesha uwiano wa kitaifa katika uteuzi wake na hivyo kuongeza ukabila, suala ambalo upinzani umesema utarekebisha.

Suala lingine ambalo mgombea wa upinzani anaahidi kutekeleza ni kuunda nafasi za kazi hasa kwa vijana lakini pia kupambana na ufisadi.

Suala la usalama, upinzani unasema utashughulikia ili kumaliza uvamizi wa kigaidi ulioshuhudiwa kipindi cha rais Uhuru Kenyatta.

Wagombea wengine

Wagombea wengine hawajaonekana sana katika vyombo vya Habari nchini humo wakifanya kampeni zao lakini, wamekuwa wakisema katika mahojiano na wanahabari kuwa  wanataka kubadilisha maisha ya Wakenya kupitia uongozi bora.

Kenya imeendelea kukabiliwa na uhaba wa unga wa mahindi, suala ambalo wanasiasa wa upinzani wameishtumu serikali kwa kushindwa kuwalisha wakenya.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.