Rais Magufuli aagiza kufutwa kazi kwa watumishi wa umma karibu 10,000
Rais wa Tanzania John Magufuli ameagiza kufutwa kazi kwa zaidi ya wafanyikazi wa karibu 10,000.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Magufuli ametoa tangazo hili siku ya Ijumaa baada ya kupokea ripoti kuhusu uchunguzi wa wafanyikazi wa serikali waliotumia vyeti gushi ili kupata kazi serikalini.
Aidha, ameitaka Wizara ya Fedha kutowalipa mshahara wafanyikazi hao waliobainika kuwa na vyeti hivyo baada ya uchunguzi kufanyika.
Kiongozi huyo ametaka majina ya wafanyikazi hao kuchapishwa katika magazeti ya nchini hiyo huku walioathirika wakitakiwa kuacha kazi mara moja.
“Watakaokataa kuondoka ikifika mwezi wa tano, watakumbana na mkono wa sheria na watafungwa jela miaka saba,” alisema Magufuli.
Katika hatua nyingine, Magufuli amesema kuwa hivi karibuni serikali yake itatangaza nafasi mpya 52,000 za kazi kwa raia wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Uamuzi huu wa rais Magufuli unakuja wakati huu dunia ikitarajiwa kuadhisha sikukuu ya Wafanyikazi tarehe 1 mwezi Mei, wiki ijayo.
Tanzania ni mojawapo ya nchi za bara la Afrika inayoendelea kukabiliwa na changamoto ya ajira haya kwa vijana.