Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA

Wanawake Kenya watakiwa kuwanyima unyumba waume zao ili wajiandikishe

Wabunge wanawake wa upinzani, wametoa wito kwa wanawake wenzao nchini humo, kuwanyima tendo la ndoa waume zao hadi pale watakapojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka huu.

Maofisa wa tume huru ya uchaguzi nchini Kenya, IEBC, wakiwa katika shughuli ya kuandikisha wapiga kura wapya, 16 Januari 2017.
Maofisa wa tume huru ya uchaguzi nchini Kenya, IEBC, wakiwa katika shughuli ya kuandikisha wapiga kura wapya, 16 Januari 2017. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Mbunge Mishi Mboko, ambaye ameolewa, amesema kuwa, wanawake wanapaswa kutofanya tendo la ndoa na waume zao hadi pale watakapowaonesha vitambulisho vya kupigia kura.

"Wanawake, kama mume wako hatajiandikisha, usimpe unyumba na mwambie akajiandikishe na kisha arudi nyumbani akiwa na kitambulisho cha kura," alisema mbunge huyo.

Wabunge hao wanawake walikuwa wakizungumza wakatik wakiwa katika kampeni zao za kisiasa kwenye eneo la pwani ya Kenya mjini Mombasa, ikiwa ni sehemu ya kampeni yao kuwahimiza raia kujitokeza na kwenda kujiandikisha tayari kwa uchaguzi wa mwezi Agosti mwaka huu.

Wabunge hao wamesema kuwa, suala la ngono ni moja ya silaha kubwa inayoweza kutumiwa na wanawake, kuwashinikiza waume zao kwenda kujiandikisha ili kufikisha idadi ya wapiga kura watakaofanya rais Uhuru Kenyatta kuondoka madarakani.

Katika hatua kama hiyohiyo, waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, nao wamegoma kuwapakia abiria ambao wanashindwa kuonesha ikiwa wanakitambulisho cha kupigia kura.

Mamlaka nchini Kenya zinakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 4 au 6 bado hawajajiandikisha idadi ambayo wadadisi wa mambo wanasema ni muhimu katika kuamua matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.