Pata taarifa kuu
TANZANIA

Maandamano ya upinzani yazusha hofu Tanzania, Polisi waonya, wapiga marufuku mikutano ya ndani

Hali ya sintofahamu ya kisiasa imezidi kuonekana nchini Tanzania ikiwa ni juma moja tu limesalia kabla ya chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA, kufanya maandamano waliyoyapa jina la UKUTA.

Polisi wa Tanzania wakijiandaa kudhibiti waandamanaji, mazoezi yao yamezusha hofu kwa wananchi.
Polisi wa Tanzania wakijiandaa kudhibiti waandamanaji, mazoezi yao yamezusha hofu kwa wananchi. DR
Matangazo ya kibiashara

Maandamano haya ya upinzani waliyosema ni ya kupinga utawala wa Udikteta nchini Tanzania, tayari yamezusha taharuki miongoni mwa wananchi, wengi wakiwa na hofu kuhusu maandamano hayo ambayo Serikali imesema haitaruhusu yafanyike.

Juma hili jeshi la Polisi nchini Tanzania, mbali na kuendelea kushikilia msimamo wake wa kutoruhusu mikutano ya kisiasa, pia limepiga marufuku kufanyika kwa mikutano yote ya ndani ya vyama, ambayo wanasema inalenga kuchochea vurugu.

Hatua ya jeshi la Polisi kupiga marufuku hata mikutano ya ndani ya vyama, imepokelewa kwa mitazamo tofauti si tu na wanasiasa lakini wananchi ambao baadhi pia wamegawanyika, ambapo wapo wanaounga mkono hatua ya Serikali na wale wanaokosoa hatua hii.

Polisi nchini Tanzania wakiwa katika mazoezi hivi karibuni, wananchi wameanza kupata hofu kuhusu mazoezi yao.
Polisi nchini Tanzania wakiwa katika mazoezi hivi karibuni, wananchi wameanza kupata hofu kuhusu mazoezi yao. DR

Upinzani umeendelea kusisitiza kuwa maandamano yao ya September Mosi yatafanyika kama yalivyopangwa na kwamba vitisho ambavyo vinaendelea kutolewa na jeshi la Polisi havitawazuia kufikia azma yao.

Haya yanajiri wakati huu wanasiasa wakongwe nchini humo, wakitoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kutafuta suluhu, huku wakimtaka Rais John Pombe Magufuli kukutana na viongozi wa upinzani kutatua sintofahamu iliyopo.

Wanasiasa hao wanasema kuwa, ikiwa Rais Magufuli atakuwa tayari kukutana na wanasiasa wenzake, basi kuna uwezekano mkubwa wa maandamano ya September Mosi kusitishwa kwa kile wanachosema kuwa, hayatakuwa na haja kwakuwa Serikali itakuwa tayari kusikiliza malalamiko yao.

Wameonya pia ikiwa Serikali ya Rais Magufuli itaendelea kupuuza madai ya upinzani, na kwamba hali hiyo itasababisha hofu zaidi na pengine kushuhudia vijana wakiingia kwenye maandamano hayo na kuna uwezekano mkubwa wa kutokea umwagikaji damu.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (katikati) akiwa na mkuu wa majeshi (kulia).
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (katikati) akiwa na mkuu wa majeshi (kulia). DR

Juma hili pia, msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, alitoa wito kwa wanasiasa nchini humo kuketi kwenye meza ya mazungumzo kuzungumzia sintofahamu iliyopo, huku mazungumzo kati yake na baraza la vyama vya siasa yakitarajiwa kufanyika kati ya Agosti 30 na 31 ya mwezi huu.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa njia pekee ya kumaliza hali tete iliyopo ni kwa wanasiasa kukutana na kuzungumzia tofauti zilizojitokeza ili kuondoa hofu kwa wananchi ambao mpaka sasa hawaelewi ikiwa maandamano hayo yatafanyika nini kitatokea.

Juma hili pia jeshi la Polisi limeshuhudiwa likifanya mazoezi ya wazi kwenye mitaa ya miji mbalimbali nchini Tanzania, ambapo wakuu wa jeshi hilo wanasema ni mazoezi ya kawaida huku wananchi wakitafsiri mazoezi hayo kama maandalizi ya kukabiliana na upinzani.

Sintofahamu hii ya kisiasa imetokana na kauli iliyotolewa na Rais John Pombe Magufuli, ambaye miezi michache iliyopita alipiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya kisiasa na badala yake akataka wabunge kufanya mikutano kwenye maeneo waliyochaguliwa na sio kuendesha operesheni za kisiasa nchi nzima.

Rais Magufuli anasema huu sio wakati wa kufanya siasa na badala yake amewataka wanasiasa wenzake pamoja na wananchi kujikita katika kufanya kazi ili kuiletea nchi maendeleo, uamuzi ambao hata hivyo umepokelewa vibaya na wanasiasa wa upinzani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.