Pata taarifa kuu
EAC-MAREKANI

Kerry: Hatuingilii uchaguzi Afrika ila hatuungi mkono uchaguzi usio huru na haki

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, katika kuhakikisha jumuiya hiyo inakuwa salama na yenyewe ustawi imara kiuchumi.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry REUTERS/Enrique Marcarian
Matangazo ya kibiashara

Waziri Kerry amesema haya jijini Nairobi nchini Kenya, ambako alikutana na mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki aliokutana nao kwa mazungumzo.

Kuhusu hali ya mambo nchini Somalia, waziri Kerry amesema Serikali yake kwa kushirikiana na vikosi vya umoja wa Afrika, AMISOM, wataendelea kushirikiana katika kuhakikisha Somalia inarejea kwenye hali ya utulivu na kundi la kigaidi la Al-Shabab linatokomezwa.

Kerry amesema kuwa, nchi yake inaunga mkono Serikali iliyoko madarakani, na kwamba watahakikisha inafanya uchaguzi mkuu wake kwa amani na utulivu, huku wakipanga kuongeza msaada wa fedha zaidi kwa vikosi vya AMISOM katika kuhakikisha usalama wa nchi hiyo.

Waziri Kerry amesema nchi yake imeendelea kufanya kazi nzuri katika vita dhidi ya Al-Shabab lakini akapongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na vikosi vya AMISOM ambayo amesema wamefanikiwa kuwafurusha kwenye maeneo mengi wapiganaji wa Al-Shabab.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry akiwa na mwenyeji wake waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Amina Mohamed walipokutaka jijini Nairobi, Agosti 22, 2016
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry akiwa na mwenyeji wake waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Amina Mohamed walipokutaka jijini Nairobi, Agosti 22, 2016 THOMAS MUKOYA / POOL / AFP

Kuhusu wakimbizi wa Somalia walioko nchini Kenya na ambao wanatakiwa kuanza kurudi nchini mwao, waziri Kerry amesema Serikali ya Kenya inapaswa kutekeleza azma yake hiyo kwa kufuata misingi ya sheria za kimataifa na nchi yake itaunga mkono kwa kuchangia zaidi ya dola za Marekani milioni 265 na nyongeza ya shilingi milioni 29.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa, wakati wa mazungumzo yake na mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi za Afrika Mashariki, wamekubaliana kubadilishana taarifa za kiintelijensia katika vita dhidi ya ugaidi, pamoja na kuongeza ulinzi zaidi kwenye maeneo ya mipaka.

Kuhusu Sudan Kusini, waziri Kerry amesema kuwa kinachoendelea kushuhudiwa kwenye taifa hilo jipya hakikubaliki, na kwamba Serikali yake inaunga mkono kwa asilimia 100 kupelekwa kwa kikosi maalumu kitakachokuwa na jukumu la kuwalinda raia na ofisi za umoja wa Mataifa.

Waziri Kerry amesema hali ya kibinadamu kwenye nchi ya Sudan hairidhishi, na ndio maana nchi yake imekubali kuchangia kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.6, kusaidia mashirika ya misaada na raia wanaokimbia nchi yao.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani, waziri Kerry amesema nchi yake haina nia yoyote na wala haitaingilia maamuzi ya Wakenya kuelekea kwenye uchaguzi huo, lakini haitakuwa tayari kuunga mkono uchaguzi ambao utakuwa hauko huru na wa haki.

Waziri Kerry amesema nchi yake itaendelea kufuatilia mchakato wa upatikanaji wa makamishana wapya wa tume ya uchaguzi, ambapo pia amepongeza uamuzi uliochukuliwa ambao ulilenga kuleta maridhiano ya kuingia kwenye uchaguzi wa mwakani kukiwa na tume inayoaminika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.