Pata taarifa kuu
BURUNDI-MAZUNGUMZO

Mazungumzo ya amani Burundi mbioni kuanza

Kikao cha kwanza cha mazungumzo ya kutafuta amani nchini Burundi kitafanyika kuanzia Mei 2 hadi 6. Mazungumzo hayo yatawakutanisha wadau wote katika mgogoro wa Burundi.

Askari polisi wakipiga doria katika kata ya Ngagara, Bujumbura, Aprili 27, 2015.
Askari polisi wakipiga doria katika kata ya Ngagara, Bujumbura, Aprili 27, 2015. AFP PHOTO / SIMON MAINA
Matangazo ya kibiashara

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa alieteuliwa na Jumuiya ya Afrika ya

Mashariki mapema mwezi uliopita kushirikiana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa kuwaweka Warundi kwenye meza ya mazungumzo kwa lengo la kutatua mzozo wa kisiasa unaoendelea katika taifa hilo ndogo la Afrika Mashariki, aliandika kwenye Twitter kwamba wadau wote watahudhuria kikao hicho cha kwanza cha mazungumzo hayo, kikao ambacho kitafanyika kuanzia Mei 2 hadi 6.

“Wadau wote wanatarajia kuhudhuria kikao cha kwanza cha mazungumzo ambacho kitafanyika mjini Arusha kuanzia tarehe 2 Mei hadi 6 Mei”, ameandika Bw Mkapa.

Afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Burundi Brigedia Jenerali Athanase Kararuza akizungumza na waandishi wa habari, Februari 5, 2014.
Afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Burundi Brigedia Jenerali Athanase Kararuza akizungumza na waandishi wa habari, Februari 5, 2014. © AFP/ISSOUF SANOGO

Hayo yanajiri wakati ambapo machafuko yanaendelea kuongezeka kila kukicha. Afisaa wa ngazi ya juu katika jeshi la Burundi, jenerali Athanase Kararuza, mkewe na mlinzi wake wameuawa mapema Jumatatu hii asubuhi wakati alipokua akielekea kazini. Jenerali Kararuza ni kutoka jeshi la zamani lililokua likitawaliwa na Watutsi. Siku moja kabla, yaani Jumapili usiku afisa mwengine kutoka jamii ya Watutsi, kanali Donatien Ndabigeze, aliponea kuuawa baada ya kushambuliwa guruneti na risasi nyumbani kwake katika kata ya Gatunguru, kaskazini mwa mji wa Bujumbura. Hata hivyo Jumapili mchana Waziri wa Haki za Binadamu wa Burundi Martin Nivyabandi na mkewe waliponea chupuchupu kuuawa baada ya kushambuliwa kwa guruneti, wakati walipokua wakitokea kanisani tarafani Nyakabiga, jijini Bujumbura.

Mazungumzo ya kutafuta amani yalifeli mwishoni mwa mwaka jana baada ya upande wa serikali kusema hauwezi kuzungumza na watu waliohusika kwa njia moja au nyingine katika jaribio la mapinduzi la mwezi Mei mwaka jana.

 ICC kuchunguza mauaji yanayoendelea

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) amesema mahakama hiyo imeanzisha uchunguzi wa awali kuhusu mauaji ambayo yamekuwa yakitokea nchini Burundi.

Bi Fatou Bensouda amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu matukio nchini Burundi tangu Aprili 2015.

“Nimekuwa nikiwatahadharisha wale wanaodaiwa kuhusika katika mauaji yanayoshughulikiwa na Mahakama ya ICC wanaweza wakawajibishwa,” amesema kupitia taarifa yake.

“Afisi yangu imetathmini mawasiliano na ripoti kadha za mauaji, kufungwa, kuteswa, ubakaji na aina nyingine za udhalilishaji wa kingono pamoja na watu kutoweka. Hivi vyote vinaonekana kuwa chini ya makosa yanayoangaziwa na ICC.”

Kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ya Haki za binadamu watu zaidi ya 500 wameuawa tangu kuanza kwa maandamano nchini humo mwezi Aprili mwaka jana. Serikali na upinzani wamekua wakitupiana lawama kila upande kuhusika na visa mbalimbali vya mauaji, mateso na ubakaji.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.