Usalama waimarishwa nje ya ubalozi wa nchi kigeni jijini Kinshasa
Nairobi – Maafisa wa usalama wameimarisha usalama nje ya ubalozi wa nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa na Umoja wa Mataifa jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia maandamano yaliyoanza kushuhudiwa wiki iliyopita na kulengwa kwa Magari yenye usajili wa kigeni, kulalamikia utovu wa usalama Mashariki mwa nchi hiyo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Polisi hapo jana wametumia mabomu ya machozi, kuwasambaratisha waandamanaji waliokuwa wanaandamana kuelekea ubalozi wa Uingereza.
Waandamanaji walivamia barabara kuu maarufu boulevard du 30 Juin, kwa lengo la kuzingira ubalozi wa Ufaransa, Marekani na ofisi za Monusco pamoja na balozi zanchi zingine za Magharibi, wakiamini kwamba nchi hizo zimeshindwa kuilaani nchi ya Rwanda inaodaiwa kuwaunga mkono waasi wa M23 mashariki mwa DRC.
‘‘Waende, tunataka waende watuwachie nchi yetu.’’ raia wa Kinshasa.
Sauti za waandamanaji jijini Kinshasa
Waziri wa mambo ya ndani Peter Kazadi, amelaani vurugu hizo.
‘‘Tungependa kuwakumbusha kwamba makazi ya wanadiplomasia wa kigeni na wafanyakazi wa MONUSCO haziwezi kushambuliwa.’’ alisema Peter Kazadi, waziri wa mambo ya ndani.
Peter Kazadi, Waziri wa mambo ya ndani wa DRC
Kama hatua ya tahadhari, shule za kigeni katika mji mkuu zimefungwa tangu asubuhi ya leo, pamoja na maduka mengi katikati mwa jiji la Kinshasa.
Freddy Tendilonge, Kinshasa rfi Kiswahili.