DRC yatiliana saini na MONUSCO kuhusu kuanza kuondoka kwa vikosi vya UN
Naiorbi – Waziri wa mambo ya nje wa DRC na kiongozi wa tume ya umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, wametiliana saini makubaliano ya kuanza kuondoka kwa walinda amani wa kimataifa waliokuwa kwenye taifa hilo kwa zaidi ya miongo miwili.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Cheza - 00:43
Waziri wa mambo ya nje, Christophe Lutundula, amesema makubaliano haya yanahitimisha rasmi ushirikiano wao na vikosi vya UN ambavyo tangu vimekuwa nchini humo vimeshindwa kurejesha usalama mashariki mwa nchi.
Katika hotuba aliyoitoa kwenye baraza la umoja wa mataifa mwezi Septemba mwaka huu, rais wa DRC, Felix Tshisekedi, alitoa wito wa kuharakishwa kwa mchakato wa kuondolewa kwa zaidi ya wanajeshi na polisi elfu 15 wa MONUSCO.
Licha ya kuwa makubaliano hayo hayakuweka wazi tarahe ya mwisho ya kuondoka kwa vikosi hivyo, wadadisi wa mambo wanasema huenda ikawa ni baada ya uchaguzi wa mwezi ujao.
Mwezi uliopita, serikali ya Kinshasa, pia iliagiza kuondoka kwa wanajeshi wa kulinda amani kutoka kikosi cha jumuiya ya Afrika Mashariki, ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Wakati huu kampeni za urais zikiwa zimeng’oa nanga, wagombea karibu wote wameonesha kuunga mkono kuondolewa kwa vikosi hivyo licha ya hali ya usalama kusalia kuwa tete katika maeneo mengi ya mashariki mwa nchi hiyo, suala hili likiwa miongoni mwa ajenga kuu za wagombea.