Pata taarifa kuu

Indonesia: Kumi na tisa wafariki katika maporomoko ya ardhi

Maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vya takriban watu 19 katika jimbo la Celebes Kusini, katikati mwa Indonesia, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha, Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga lilitangaza Jumapili hii, Aprili 14.

Waokoaji wakiwatafuta manusura kwenye vifusi vya hospitali ya Mitra Manakarra katika mji wa Mamuju, katika kisiwa cha Celebes, iliyokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi, Januari 15, 2021.
Waokoaji wakiwatafuta manusura kwenye vifusi vya hospitali ya Mitra Manakarra katika mji wa Mamuju, katika kisiwa cha Celebes, iliyokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi, Januari 15, 2021. AFP - FIRDAUS
Matangazo ya kibiashara

"Jumla ya watu 19 wamefariki baada ya kuzikwa kwenye maporomoko ya udongo katika wilaya ya Tana Toraja mkoa wa Sulawesi Kusini," Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga limesema. Maporomoko hayo yametokea usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili.

Miili ya waliofariki na wawili walionusurika waliondolewa kwenye chini ya matope baada ya janga kukumba vijiji vya eneo la Tana Toraja katika jimbo hili Jumamosi jioni, amesema Sulaiman Malia, Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga katika eneo hilo.

"Kuna vifo 19, 4 huko Makale Kusini na vingine 15 katika vijiji vinavyozunguka Makale," ameliambia shirika la habari la AFP katika ripoti iliyosasishwa. "Kwa sasa, bado tunatafuta waathiriwa wengine," ameongeza, akibainisha kuwa watu wawili walikuwa bado hawajapatikana, labda walizikwa kwenye maporomoko ya udongo.

Tana Toraja na maeneo yanayoizunguka "yameathiriwa na mvua kubwa, haswa katika wiki iliyopita, bila kukata" aliongeza.

Mvua kubwa iliyonyesha ilimomonyoa udongo katika maeneo ya makazi ya watu kando ya mlima, na kusababisha maporomoko ya ardhi yaliyozika makazi ya wakazi, amesema.

Indonesia hukumbwa na maporomoko mengi ya ardhi wakati wa msimu wa mvua na hali hiyo imekuwa mbaya zaidi katika baadhi ya maeneo kutokana na ukataji miti.

Mapema mwezi Machi, mafuriko na maporomoko ya ardhi katika kisiwa cha Sumatra yalisababisha vifo vya takriban watu 30 na wengine kadhaa kukosekana.

Mwezi wa Desemba mwaka jana, maporomoko ya ardhi na mafuriko yalisomba nyumba nyingi na kuharibu hoteli karibu na Ziwa Toba huko Sumatra, na kuua watu wasiopungua wawili.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.