Pata taarifa kuu

Bangladesh: Makabiliano yazuka kati ya polisi na wafanyakazi wa viwanda vya nguo

Makabiliano mapya yamezuka kati ya polisi na wafanyakazi wa tasnia ya nguo Jumamosi asubuhi, wakati wa kufungua tena viwanda vya nguo. Takriban viwanda 600 vinavyozalisha nguo kwa makampuni makubwa ya mavazi duniani vimeanza kazi tena, baada ya kufungwa kwa takriban wiki moja na wafanyakazi wanaodai nyongeza ya mishahara.

Polisi wa Bangladesh wanamzuilia mwanamume mmoja walipokuwa wakiwatawanya wafanyakazi wa kiwanda cha nguo nchini Bangladesh waliokuwa wakizuia usafiri wa magari wakidai ujira bora zaidi katika eneo la Dhaka-Mirpur nchini Bangladesh, Alhamisi, Nov.2, 2023.
Polisi wa Bangladesh wanamzuilia mwanamume mmoja walipokuwa wakiwatawanya wafanyakazi wa kiwanda cha nguo nchini Bangladesh waliokuwa wakizuia usafiri wa magari wakidai ujira bora zaidi katika eneo la Dhaka-Mirpur nchini Bangladesh, Alhamisi, Nov.2, 2023. AP - Mahmud Hossain Opu
Matangazo ya kibiashara

Takriban wafanyakazi 10,000 kutoka viwanda vya kuzalisha nguo wamejaribu kuwazuia wenzao kurejea kazini katika mji wa viwanda wa Ashulia, katika vitongoji vikubwa vya magharibi mwa mji mkuu Dhaka. Wamerusha mawe na matofali kwa vikosi vya polisi vilivyotumwa kwa wingi - waandamanaji hao pia wamejaribu kufunga barabara na njia za kuingia viwandani - kabla ya kutawanywa kwa mabomu ya machozi.

Miongoni mwa mamia ya viwanda vilivyofungwa ni "viwanda vikubwa zaidi nchini, ambavyo vinasambaza bidhaa zote kuu kwenda nchi za Magharibi", kulingana na Kalpona Akter, kiongozi wa Shirikisho la wafanyakazi wa viwandai vya kuzalisha Nguo na mavazi nchini Bangladesh. Viwanda hivi vinasambaza chapa au wasambazaji kama vile "Gap, Walmart, H&M, Zara, (kampuni) Inditex (ambayo Zara ni sehemu yake), Bestseller, Levi's, Marks na Spencer, Primark et Ald".

Kazi imeanza tena katika karibu viwanda 600, hasa katika mji wa viwanda wa Gazipur, ambapo maandamano yalikuwa na vurugu. Katika siku za hivi karibuni, wafanyakazi wasiopungua wawili waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa kando ya vuguvugu hili la maandamano lililoanza mwishoni mwa mwezi Oktoba. Viwanda vingi pia vimeharibiwa, au hata kuchomwa moto... Wafanyakazi wa viwanda vya kuzalisha nguo nchini Bangladesh wanashutumu kutumiwa vibaya na makampuni makubwa kutoka nchi za Magharibi.

Wakikabiliwa na mfumuko wa bei na kupanda kwa kasi kwa gharama za chakula, wanadai ongezeko kubwa la mishahara yao ya kila mwezi, lakini shirika la waajiri la wazalishaji linapendekeza tu ongezeko la 25%. Wafanyakazi hao wanadai nyongeza hadi taka (fedha za Bangladesh) 23,000 kwa mwezi, karibu mara tatu zaidi ya taka 8,300 za kima cha chini cha sasa cha mshahara (takriban euro 70 kwa mwezi).

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.