Ni kosa kwa wanawake kutembea bila kufunika nyuso zao- Taliban
Uongozi wa kundi la Taliban nchini Afghanistan, umewaagiza wanawake kwenye taifa hilo kufunika nyoso zao kwa burqa wakati wakiwa katika maeneo ya umaa.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Agizo hili limetajwa kuwa moja wapo ya marshati makali zaidi kutangazwa na kundi hilo dhidi ya wanawake nchini Afghanistan tangu kuchukua uongozi wa taifa hilo mwaka jana, Baadhi ya sheria zinazotekelezwa na wapiganaji hao zimekuwa zikikashifiwa vikali na jamii ya kimataifa pamoja na raia kwenye taifa hilo.
Haibatullah Akhunzada, Mkuu wa kundi la Taliban katika taarifa yake iliyosomwa wakati wa halfa iliyofanyika jijini Kabul siku ya jumamosi, ametaja kitendo cha wanawake kujifunika kutoka kichwani hadi kwenye miguu kuwa kitendo kinachoaashiria heshima katika jamii na kinalinagana na tamaduni.
Agizo hilo aidha linaeleza kuwa iwapo baba au mtu mwenye jinsia ya kiume na ambaye ni wa karibu na mwanamke atakayepatikana katika maeneo ya umma bila ya kujifunika uso wake, “atatembelewa” na kufungwa jela au hata kuaachishwa kazi kwa wale walioaajiriwa na serikali.
Tangu kuchukua madaraka, Taliban wamerejesha baadhi ya sheria zikiwemo kudhibiti uhuru wa watu kutembea sheria zinazowalenga wanawake pakubwa hali inayorejesha picha ya utawala wao katika miaka ya 1990.
Kwa kipindi cha miezi michache iliyopita, viongozi wa Taliban wametangaza marsharti na vikwazo vingi kwa raia wa Afghanistan licha ya kukashifiwa na jamii ya kimataifa.
Mwezi disemba mwaka jana, Taliban ilitangaza sheria inayowazuia wanawake kwenda umbali wa kilomita 72 bila ya kuaandamana na mtu wa jinsia ya kiume.
Marekani na mataifa mengine yamesitisha msaada kwa Afghanistan tangu wapiganaji wa Taliban walipochukua uongozi mwezi agosti na hata kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo.