Visanduku vyeusi vya AirAsia vyapatikana
Wapiga mbizi nchini Indonesia wamethibitisha kupatikana kwa visanduku vyeusi vya kurekodi data na sauti vya ndege ya AirAsia ambayo ilianguka katika bahari ya Java.
Imechapishwa:
Wataalamu wa kimataifa, hata hivyo, wamesema hawajaweza kuviondoa kutoka chini ya bahari kwa sababu vimekwama kati ya vipande viwili vya ndege hiyo.
Wizara ya uchukuzi ya Indonesia imesema, leo Jumatatu kuwa watalaamu hao wanatarajiwa kukiondoa majini kipande cha ndege hiyo kwa kutumia mifuko maalum ya majini na kuviondoa visanduku hivyo.
Maafisa wanaamini kuwa wahanga wengi wa ajali hiyo bado wamekwama ndani ya kipande cha katikati cha ndege hiyo. Jumapili Januari 11, kipande cha mkia kiliondolewa majini lakini wataalamu hawakupata visanduku hivyo vya kurekodi mawasiliano.
Kufikia sasa miili 48 kati ya watu 162 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo imepatikana.