Pata taarifa kuu

Lavrov aishukuru Brazil kwa juhudi zake za kuleta amani nchini Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov hivi punde ameishukuru Brazil kwa "mchango" wake katika kutafuta suluhu la mzozo wa Ukraine, kabla ya mkutano wake uliopangwa kufanyika na Rais Lula mjini Brasilia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov. © Alexander Zemlianichenko / AP
Matangazo ya kibiashara

Wiki iliyopita, wakati wa ziara rasmi nchini China, Luiz Inacio Lula da Silva alitangaza kwamba Marekani lazima ikome "kuhimiza" mgogoro huu. Chanzo kutoka ofisi ya rais kimelithibitishia shirika la habari la AFP kwamba mkutano kati ya Lula na Bw. Lavrov ulifanyika saa 17:00 kwa saa za huko (sawa na 8:00 p.m. GMT), katika Ikulu ya Alvorada, makazi rasmi ya mkuu wa nchi wa Brazil.

Kabla ya mkutano huu, mkuu wa diplomasia ya Urusi, ambaye mamlaka ya Brazil ilimtandazia zulia jekundu kwenye uwanja wa ndege wa Brasilia, alizungumza mchana na mwenzake Mauro Vieira.

"Tunaishukuru Brazil kwa mchango wake katika (kutafuta) suluhisho la mzozo huu," alisema katika mkutano na waandishi wa habari. "Tuna nia ya kuona mzozo huu unamalizika haraka iwezekanavyo," aliongeza, huku akitetea, hata hivyo, suluhisho "la kudumu na sio la haraka". Wiki iliyopita, Lula alisisitiza nia yake ya kuunda "kundi la G20 la kutafuta amani", kundi la nchi ambazo lengo lao litakuwa kufanya kazi ya kumaliza mzozo wa Ukraine.

Pia alisema kuwa Marekani inapaswa "kuacha kuhimiza vita na kuanza kuzungumza kuhusu amani". Na "Umoja wa Ulaya lazima uanze kuzungumza juu ya amani", alisema rais wa Brazil Jumamosi mbele ya waandishi wa habari huko Beijing. Siku iliyofuata, wakati alipotua katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Lula alibaini kwamba vita vilivyoanzishwa na Urusi dhidi ya Ukraine mnamo mwezi Februari 2022 vilisababishwa na 'maamuzi yaliyochukuliwa na nchi mbili'.

"Tunashukuru kwa marafiki zetu wa Brazili kwa uelewa mzuri wa mwanzo wa hali hii" huko Ukraine, alisema Bw. Lavrov Jumatatu huko Brasilia. "Tumeunganishwa na nia ya pamoja ya kuunda ulimwengu wa usawa," aliongeza.

Siku kumi zilizopita, nchini Uturuki, albainisha kwamba mazungumzo ya amani juu ya Ukraine yanawezekana tu ikiwa yanalenga kuanzishwa kwa "utaratibu mpya wa dunia", bila kutawaliwa na Marekani. Ziara ya Bw. Lavrov mjini Brasilia inakuja wiki tatu baada ya ile ya mjini Moscow ya Celso Amorim, mshauri mkuu wa Rais Lula wa masuala ya kimataifa, ambaye alikutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin huko Kremlin.

Brazil na Urusi ni sehemu ya BRICS, kundi la nchi zinazoinukia ambazo pia zinajumuisha India, China na Afrika Kusini katika safu zake. Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Urusi TASS, Brazil ni hatua ya kwanza ya ziara ya wiki moja ya Bwana Lavrov katika Amerika ya Kusini, ikiwa ni pamoja na Venezuela, Nicaragua na Cuba, nchi tatu zinazoonyesha msimamo wao waziwazi dhidi ya Washington.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.