Mexico: Mwandishi wa habari Alfredo Cardoso Echeverria auawa kwa risasi
Mkurugenzi wa tovuti ya habari huko Acapulco, katika jimbo la Guerrero, kusini mwa Mexico, alifariki Oktoba 31 hospitalini, siku mbili baada ya kupatikana akiwa amejeruhiwa vibaya kwa risasi, mamlaka imetangaza.
Imechapishwa:
"Ninapaswa nitoe rambirambi zangu kwa familia ya mwanahabari Alfredo Cardoso Echeverria, mwanzilishi wa tovuti ya habari ya Las Dos Costas, kwa mauaji haya ya kusikitisha," Evelyn Salgado, gavana wa jimbo la Guerrero, alisema kwenye mtandao wa kijamii.
Kulingana na shirika la Wanahabari Wasio na Mipaka (RSF), Bw. Cardoso, ambaye familia yake ilipokea vitisho, alitekwa nyara Alhamisi (Oktoba 28) na watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao ambao walivamia nyumba yake.
Alipatikana siku iliyofuata akiwa amejeruhiwa kwa risasi tano kwenye gari lake, vyombo vya habari vya nchini Mexico vimeripoti. Alikimbizwa hospitalini haraka, mwanahabari huyo alifariki dunia siku ya Jumapili.
Takriban wanahabari saba wameuawa mwaka huu wa 2021 nchini Mexico. Lakini, haijbainishwa kuwa vifo vyao vilihusiana na kazi yao.
Mexico, ikiwa na zaidi ya waandishi wa habari mia moja waliouawa tangu mwaka 2000 kulingana na takwimu kutoka Tume ya Haki za Kibinadamu, inachukuliwa kuwa moja ya nchi hatari zaidi kwa wale wanaofanya kazi ya kuelimisha umma.
Waandishi wanane waliuawa mnamo 2020, RSF imekumbusha. Zaidi ya 90% ya mauaji ya waandishi wa habari hayaadhibiwi, mashirika yanayotetea uhuru wa kujieleza yanabaini.