Pata taarifa kuu
MAREKANI-BIDEN-SIASA

Biden amteua mwanamke wa kwanza mweusi Kamala Harris kuwa mgombea mwenza

Mgombea urais kupitia chama cha Democratic nchini Marekani Joe Biden, amemteua Seneta wa California Kamala Harris, kuwa mgombea mwenza wakati wa uchaguzi wa urais utakaofanyika mwezi Novemba.

Joe Biden na Kamala Harris.
Joe Biden na Kamala Harris. REUTERS/Lucas Jackson
Matangazo ya kibiashara

Uteuzi wa Bi Harris, unamaliza subira ya miezi kadhaa kufahamu ni nani atakuwa mgombea mwenza wa Biden, ambaye atapambana na rais Donald Trump.

Harris ambaye pia aliwahi kutia nia ya kutaka kuwa mgombea urais, iwapo chama cha Democratic kitashinda, anatarajiwa kuwa makamu wa rais wa kwanza Mwanamke mweusi mwenye asili ya India.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa Harris mwenye umri wa miaka 55 ambaye ana historia ya kubaguliwa kwa sababu ya rangi yake na kuwa mpambanaji, anatarajiwa kuvutia wapigakura wanaohisi kutothaminiwa nchini Marekani.

Katika historia ya siasa nchini Marekani, Bi Harris anakuwa mgombea wa tatu mwanamke, akitanguliwa na Geraldine Ferraro mwaka 1984 na Sarah Palin mwaka 2008.

Harris amesema ameheshimika sana kuteuliwa kama mgombea mwenza na atafanya kila analoweza kumsaidia, Biden kushinda Uchaguzi huo na kumwelezea kama kiongozi aliye na uwezo wa kuwaunganisha Wamarekani.

Rais Trump amesema ameshangazwa na uteuzi wake, licha ya kufanya vibaya katika kura za kutafuta ugombea wa urais kupitia chama cha Demoratic.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.