Bolivia: Evo Morales marufuku kuwania katika Uchaguzi wa maseneta
Rais wa zamani wa Bolivia Evo Morales amepigwa marufuku kuwania katika uchaguzi wa maseneti, uamuzi ambao umechukuliwa taasisi kuu ya uchaguzi nchini Bolivia.
Imechapishwa:
Hatua hii inahatarisha kurudi kwake kisiasa baada ya kujiuzulu mwezi Novemba.
Mahakama Kuu ya Uchaguzi ya Bolivia (TSE) imebaini kwamba Evo Morales hajatimiza wajibu wa "makazi ya kudumu" nchini Bolivia.
Evo Morales aliondoka Bolivia kwenda Mexico baada ya kujiuzulu mwezi Novemba, baada ya wiki kadhaa za maandamano dhidi yake na chini ya shinikizo kutoka kwa vikosi vya jeshi, kufuatia uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata. Kisha akakimbilia Argentina.
Uamuzi wa Mahakama "ni pigo dhidi ya demokrasia. Wajumbe (wa mahakama hii) wanajua kuwa ninatimiza masharti ya kuwa mgombea. Malengo yao ni kukifuta kabisa chama cha MAS", amebaini Bwana Morales kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Kwa upande wake, mpinzani wake mkuu, Rais wa zamani Carlos Mesa amekaribisha uamuzi wa mahakama, akisema, "sheria na Katiba vimetumiwa kwa usahihi". Evo Morales "anapaswa kuelewa kuwa hawezi tena kutumia sheria kulingana na masilahi yake," ameongeza.
Chama cha Bw. Morales, MAS, hata hivyo kitawakilishwa katika uchaguzi wa urais. Waziri wa zamani wa Uchumi, Luis Arce, amekubaliwa na Mahakama Kuu ya Uchaguzi kuwania katika uchaguzi wa urais, Mkuu wa mahakama hiyo Salvador Romero alisema Alhamisi katika mkutano na waandishi wa habari.
Aliteuliwa rasmi kupeperusha bendera ya chama cha MAS Februari 9, 2020.