Rais Maduro ataka katiba mpya, upinzani wakataa
Siku ya Jumatatu rais wa Venezuela Nicolas Maduro alitoa wito wa kuundwa kwa Bunge la Katiba, ambalo litakua na mamlaka ya kuandika katiba mpya. Licha ya tangazo hilo, maandamano yaliendelea kushuhudiwa katika mitaa mbalimbali nchini Venezuela.
Imechapishwa:
Rais Maduro amesema taasisi hiyo mpya itaundwa na raia wa kawaida na kuachana na bunge la kitaifa lenye wabunge wengi kutoka upinzani.
Wakati huo huo kiongozi wa upinzani Henrique Capriles amesema taasisi hiyo itakua na malengo ya kufuta katiba ya nchi.
Hayo yakijiri maelfu ya wafuasi wa upinzani walimiminika siku ya Jumatatu mitaani wakidai kufanyike uchaguzi wa mapema, hata hivyo makabiliano makali yalishuhudiwa kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.
Venezuela imeendelea kukumbwa na maandamano ya upinzani wakitaka rais Nicolas maduro ajiuzulu mara moja.