Pata taarifa kuu
HAKI-SIASA

Afrika Kusini: Baada ya kutengwa kushiriki uchaguzi, rais wa zamani Zuma akata rufaa

Rais wa zamani Jacob Zuma amekata rufaa Jumanne kupinga kuenguliwa kwake kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Mei nchini Afrika Kusini, na kuibua mjadala kuhusu kustahiki kwake chini ya miezi miwili kabla ya uchaguzi huo ambao unaonekana kuwa na mvutano.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma mnamo Aprili 17, 2023 katika mahakama ya Pietermaritzburg.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma mnamo Aprili 17, 2023 katika mahakama ya Pietermaritzburg. © Kim Ludbrook / AP
Matangazo ya kibiashara

Raia wa Afrika Kusini watapiga kura Mei 29 kuwachaguwa wabunge wao, ambao watamchagua rais ajaye. Jacob Zuma, 81, alikuwa mgombea katika orodha ya chama kilichoundwa hivi karibuni kiitwacho Umkhonto We Sizwe (MK, mkuki wa taifa kwa Kizulu).

Nguzo ya zamani ya chama cha African National Congress (ANC), kilichoko madarakani kwa miaka thelathini, ilizua mshangao mwezi Desemba kwa kutangaza kuunga mkono chama kidogo cha itikadi kali, wakati ambapo ANC inahofia kupoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza katika uchaguzi huo.

Mara kwa mara akiwaita wanachama wa ANC "wasaliti", adui wa kisiasa wa Rais Cyril Ramaphosa amerejelea kauli yake kwamba "haitambui tena chama" ambacho alipigana dhidi ya ubaguzi wa rangi, na kutoa wito kwa umma "kuirudisha nchi" kwa kujiunga na safu ya chama cha MK. Lakini siku ya Alhamisi, tume ya uchaguzi (IEC) ilibatilisha ugombea wa Bw. Zuma. Haikueleza sababu waziwazi, ikisema tu kwamba ilipokea "pingamizi ambalo lilizingatiwa".

Tume ilikariri mara moja masharti ya kustahiki mgombea kwa mujibu wa Katiba, ikisisitiza hasa kwamba mtu aliyehukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi 12 hawezi kuwania katika uchaguzii. Hata hivyo, Jacob Zuma, aliyeshitakiwa katika kesi kadhaa za rushwa, alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela kwa kosa la kudharau mahakama mwaka 2021.

Bw. Zuma "hajakabiliwa na mashtaka ya jinai na wala hajawahi kufunguliwa mashtaka ya jinai", imehoji MK katika rufaa yake iliyowasilishwa kwenye Mahakama ya Uchaguzi na ambayo shirika la habari la AFP limepata nakala yake. Kwa kuhoji kutopendelea kwa tume ya uchaguzi, chama hicho kinaamini kuwa kesi iliyompeleka bwana Zuma gerezani ni ya "utaratibu wa kiraia".

Pia kinakumbuka kwamba akiwa jela Julai 2021, Jacob Zuma aliruhusiwa kuachiliwa kwa masharti kwa sababu za kiafya baada ya zaidi ya miezi miwili. "Rais Ramaphosa alimpa msamaha, na hivyo kupunguza kifungo chake cha mwisho," chama cha MK kinasema.

Uchaguzi huo unaonekana kuwa na mvutano kwa ANC, ambayo inapoteza kasi kutokana na kashfa nyingi na kutokuwa na uwezo wa kufufua uchumi ulioyodorora. Kulingana na kura za hivi punde, chama hicho cha kihistoria kitashinda zaidi ya 40% ya kura, ikilinganishwa na 27% ya kura kwa chama cha kwanza cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) na 13% kwa chama cha MK. Kwa hivyo chama cha ANC kitapoteza, kwa mara ya kwanza, wingi wake wa wabunge na kinaweza kujikuta kikilazimishwa kuunda serikali ya mseto.

Katika wiki za hivi karibuni, mvutano umeongezeka kati ya ANC na MK. Chama tawala kilijaribu kuondoa chama hiki kutoka kwa orodha ya vyama vilivyosajiliwa kwa uchaguzi huo, lakini mahakama wiki iliyopita ilikataa rufaa hiyo, ikizingatiwa kuwa hoja za upande wa mashitaka zilikuwa hazitoshi.

Chama cha ANC kimewasilisha rufaa nyingine kukitaka chama cha Jacob Zuma kubadili jina na nembo yake, kikilaani "wizi wa mali miliki na urithi". MK asili ni jina la tawi la kijeshi la chama cha ANC wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa wazungu. Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi wake siku chache zijazo.

Kauli mbaya za wanachama wa MK hivi karibuni zimesababisha wasiwasi miongoni mwa mamlaka. "Ikiwa mahakama hizi, ambazo wakati mwingine 'zinadhibitiwa', zitasimamisha MK, kutakuwa na machafuko nchini. Kutakuwa na ghasia ambazo hujawahi kuona," alionya Visvin Reddy, afisa mkuu wa chama, katika video iliyoshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kufungwa kwa Jacob Zuma mwaka 2021 kulifuatiwa na wimbi la ghasia na uporaji ambao haujawahi kutokea nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi mwaka 1991, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 350. Orodha za mwisho za uchaguzi zinatarajiwa kuchapishwa wiki ijayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.