Pata taarifa kuu
MAANDAMANO-DIPLOMASIA

Niger: Maelfu ya wananchi wataka wanajeshi wa Ufaransa kuondoka

Nchini Niger, siku ya pili ya maandamano Jumamosi hii Septemba 2 kudai kuondoka kwa jeshi la Ufaransa. Maelfu kadhaa ya waandamanaji wameitikia mwito wa M62, muungano wa mashirika ya kiraia ambayo yanaunga mkono mapinduzi ya kijeshi ya Julai 26 na yanayotaka kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa nchini humo. Maandamano yamefanyika huko Ouallam, kusini-magharibi, na hasa Niamey.

Mmoja wa waandamanaji ameshikilia fulana iliyoandikwa "Ufaransa lazima iondoke", wakati wafuasi wa Baraza la Kitaifa la ulinzi wa nchi (CNSP) wakiandamana mbele ya kambi ya kikosi cha jeshi la wanaanga huko Niamey Jumamosi hii, Septemba 2, 2023.
Mmoja wa waandamanaji ameshikilia fulana iliyoandikwa "Ufaransa lazima iondoke", wakati wafuasi wa Baraza la Kitaifa la ulinzi wa nchi (CNSP) wakiandamana mbele ya kambi ya kikosi cha jeshi la wanaanga huko Niamey Jumamosi hii, Septemba 2, 2023. AFP - -
Matangazo ya kibiashara

Makumi ya maelfu ya waandamanaji walikusanyika kwenye randabauti ya Escadrille, mbele ya kambi ya jeshi la Niger katika mji mkuu wa Niger, Niamey, ambapo wanajeshi wa Ufaransa wanapaiga kambi.

Waandamanaji, ambao wengi wao ni vijana, wameandamana na mabango na kuimba zinazopinga Ufaransa na jeshi lake, wakitaka wanajeshi wa Ufaransa waondoke "mara moja" na "bila masharti".

Hakuna makabiliano yoyote yaliyotokea, lakini picha zilizorushwa na vyombo vya habari vya Niger au na waandamanaji wenyewe kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha kwamba wakati mwingine polisi walikuwa na ugumu wa kudhibiti umati wa watu na kuwazuia waandamanaji kuingia kwenye kambi hiyo.

Mwanzoni mwa mwezi huu, wanajeshi waliochukua mamlaka nchini Niger walishutumu makubaliano ya ulinzi juu ya "kuishi" na "hadhi" ya askari wa Ufaransa.

Kuna takriban wanajeshi 1,500 wa Ufaransa nchini humo. Na walikuwa, kabla ya mapinduzi, wakishirikiana na vikosi vya Niger dhidi ya wanajihadi wa Al-Qaeda na kundi la Islamic State.

Lakini askari wa CNSP hawataki tena ushirikiano huo. Utawala mpya unaishutumu Ufaransa kwa kusaidia makundi ya kigaidi.

Walakini, Paris hadi sasa imesalia kimya. Ufaransa haitambui CNSP, inachukulia maamuzi yake kuwa haramu na inakataa kuyazingatia. Siku ya Jumamosi asubuhi Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, amesisitiza kwenye vyombo vya habari: suala la kuondoka kwa kikosi cha Ufaransa nchini Niger halimo kwenye programu.

Kumbuka kwamba mvutano kama huo, unashuhudiwa dhidi ya balozi wa Ufaransa, ambaye CNSP inapanga kumfukuza baada ya kumvua kibali chake. Kwa hivyo hali ni ya wasiwasi zaidi kuliko hapo awali na inaonekana kuwa itaendelea. Siku ya tatu ya maandamano imepangwa Jumapili hii.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.