Pata taarifa kuu

Tunisia: Makabiliano yaripotiwa kati ya Watunisia na wahamiaji Sfax

Mahakama imefungua uchunguzi siku ya Jumatatu kufuatia makabiliano kati ya wahamiaji haramu kutoka nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na wakaazi wa Sfax, mji wa pili kwa ukubwa nchini Tunisia ambapo uhamiaji haramu umekuwa ukisababisha mvutano mkubwa kwa miezi kadhaa.

Wakazi wa Kusini mwa Jangwa la Sahara wakijiandaa kuchukua ndege kuondoka Tunis na kuhamishwa baada ya wimbi la ghasia za ubaguzi wa rangi nchini humo, Machi 4, 2023.
Wakazi wa Kusini mwa Jangwa la Sahara wakijiandaa kuchukua ndege kuondoka Tunis na kuhamishwa baada ya wimbi la ghasia za ubaguzi wa rangi nchini humo, Machi 4, 2023. © FETHI BELAID / AFP
Matangazo ya kibiashara

Makabiliano hayo, ya kurushiana mawe, yalihusisha wahamiaji dhidi ya wakaazi wa wilaya ya Rabd, msemaji wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa Sfax, Faouzi Masmoudi, ameliambia shirika la habari la AFP. Magari na nyumba ziliharibiwa wakati wa makabiliano, ambayo hayakusababisha majeruhi, Masmoudi amesema. Uchunguzi umefunguliwa ili kubaini waliohusika na sababu za ghasia hizi, ameongeza.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, maafisa wa polisi waliingilia kati kwa kutumia vitoa machozi ili kukomesha mapigano hayo. Sfax, katikati-mashariki mwa Tunisia, ndio mahali pa kuanzia kwa idadi kubwa ya vivuko haramu kwenda Italia. Wakazi wake huandamana mara kwa mara dhidi ya uwepo wa wahamiaji haramu katika jiji lao na kutaka waondoke.

Katika vitongoji maarufu vya jiji ambako wahamiaji wanaishi, vurugu za matusi na kimwili mara nyingi huzuka kati ya pande hizo mbili. Ghasia hizi ziliongezeka baada ya hotuba ya Rais Kais Saied, Februari 21, akishutumu uhamiaji haramu na kuuonyesha kama tishio la kukuwa kwa idadi ya watu kwa nchi yake.

Wakati huo huo mashirika kadhaa yasio ya kiserikali ya ndani na ya kimataifa yalishutumu "hotuba za chuki na vitisho dhidi ya wahamiaji (kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara) zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinachangia uhamasishaji dhidi ya makundi yaliyo hatarini zaidi na kuchochea tabia ya ukatili dhidi yao." Mwishoni mwa mwezi Mei, mhamiaji wa Benin mwenye umri wa miaka 30 aliuawa kwa kuchomwa kisu wakati wa shambulio lililotekelezwa na kundi la vijana wa Tunisia katika kitongoji cha maarufu huko Sfax.

Wahamiaji wengi kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara huja Tunisia kisha kujaribu kuingia Ulaya kwa njia ya bahari, wakitua kwa siri kwenye pwani ya Italia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.