Pata taarifa kuu
AFYA - VIRUSI VYA MARBURG

Tanzania yatangaza tahadhari ya usafiri baada ya virusi vya Marburg

Wizara ya afya nchini Tanzania, imesema abiria wote wanaotoka katika eneo la Kagera, watalazamika kujaza fomu maalum ili kusaidia kudhibiti ugonjwa huo.

Mtazamo wa chembe za virusi vya Marburg chini ya darubini ya elektroni
Mtazamo wa chembe za virusi vya Marburg chini ya darubini ya elektroni Centers for Disease Control and Prevention
Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili la wizara ya afya, limekuja kufuatia tangazo la kuzuka kwa virusi vya Marburg mnamo Machi 22, Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo, na kusababisha vifo vya watu watano. 

Maabara ya taifa ya afya ya umma ya Tanzania, ilichunguza sampuli ili kubaini chanzo cha ugonjwa baada ya watu wanane kupata dalili zikiwemo homa, kutapika, kutokwa na damu na kufeli kwa figo.

Nayo wizara ya afya nchini Kenya, imetoa taarifa ikisema imechukua tahadhari mipakani kuzuia maambukizi hayo wakati huu sekta ya afya nchini humo ikiwa angalifu. Davji Bhimji Atella ni daktari nchini Kenya na pia Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari nchini humo akielezea ugonjwa huu.

Iko na zile dalili ambazo zinafanana na za Ebola, ambapo unakuwa na maumivu ya misuli na pia kuharisha. Mara nyingi milipuko ambayo imetokea katika nchi tofauti imekuwa na hizo dalili, lakini ile ambayo ni hatari,  ni kila sehemu ya wazi mwilini kutokwa na damu. Amesema daktari Atella.  

Tathmini ya kimkakati iliyofanywa na shirika la Afya Dunia WHO, mnamo Septemba 2022, ilionyesha kuwa nchi ya Tanzania iko katika hatari kubwa sana ya kuzuka kwa magonjwa ya kuambukiza.

Guinea ya Ikweta

Siku ya Alhamisi, Shirika la afya duniani WHO, lilisema virusi hivyo vya Marburg, vimeua watu 20 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita nchini Guinea ya Ikweta.

Kwa mujibu wa serikali, mlipuko huo ambao ni hatari kama ule wa Ebola, umeenea zaidi ya mkoa wa Kie-Ntem, ambapo ulisababisha kifo cha kwanza mwezi Januari na umefika hadi mji wa kibiashara wa Bata.

Mkurugenwzi wa WHO, barani Afrika, Dr Matshidiso Moeti, amesema kusambaa kwa virusi hivyo, ni dalili tosha ya kuongeza juhudi ili kukomesha maambukizi na kuepusha uwezekano wa mlipuko mkubwa na kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa WHO, kwa sasa hakuna chanjo dhidi ya virusi hivyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.