Pata taarifa kuu
HAKI-SHERIA

Mauaji ya balozi wa Italia nchini DRC: Washtumiwa wakabiliwa na adhabu ya kifo

Ofisi ya mashitaka ya kijeshi mjini Kinshasa siku ya Jumatao, imeomba hukumu ya kifo dhidi ya wanaume sita walioshitakiwa mbele ya mahakama ya kijeshi kwa mauaji ya balozi wa Italia, mlinzi wake na dereva mnamo Februari 2021 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa wamebeba miili ya waliouawa katika shambulizi huko Nyiragongo, Kivu Kaskazini, ukiwemo mwili wa Balozi wa Italia, Luca Attanasio, Februari 22, 2021.
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwa wamebeba miili ya waliouawa katika shambulizi huko Nyiragongo, Kivu Kaskazini, ukiwemo mwili wa Balozi wa Italia, Luca Attanasio, Februari 22, 2021. © Justin Kabumba / AP
Matangazo ya kibiashara

Adhabu ya kifo mara nyingi huombwa na kutolewa nchini DRC katika kesi za usalama wa taifa, lakini haijatumika kwa miaka 20 na inabadilishwa kwa utaratibu kuwa kifungo cha maisha.

"Waathiriwaa walitekwa nyara, wakaburutwa ndani kabisa ya msitu kabla ya kuuawa," mwendesha mashtaka wa kijeshi, Kapteni- Hakimu Bamusamba Kabamba, katika mashitaka yake mbele ya mahakama ya kijeshi ya Kinshasa-Gombe, kesi iliyosikilizwa katika jela la kijeshi la Ndolo. Washtakiwa watano kati ya sita wanazuiliwa katika gereza hili, lakini mmoja yuko mafichoni. Wote sita wanakabiliwa na adhabu ya kifo.

Washtumiwa hao ambao wanashtakiwa kwa "mauaji, kushirikiana na kundi la wahalifu, kumiliki silaha kinyume cha sheria na risasi za kivita", wamekuwa wakishtakiwa tangu Oktoba 12 kwa mauaji ya Februari 22, 2021 ya balozi wa Italia nchini DRC, Luca Attanasio, mlinzi wake, raia wa Italia, Vittorio Iacovacci, na dereva wa shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, Mustapha Milambo.

Watu hao watatu waliuawa kwa kupigwa risasi baada ya kuanguka katika shambulizi la kuvizia karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Virunga, katika mkoa wa Kivu Kaskazini (mashariki), eneo linalokumbwa na ghasia kutoka kwa makundi yenye silaha kwa takriban miaka 30.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwataja washtakiwa hao kuwa ni wanachama wa "genge la uhalifu" na majambazi wa barabara kuu, ambao awali hawakukusudia kumuua balozi huyo, bali kumteka nyara na kutaka dola milioni moja ili aachiliwe. Washtakiwa waliokuwepo, ambao walikamatwa mwezi Januari 2022, wamekuwa wakikanusha madai hayo wakati wote wa kesi, wakipinga ushahidi wao wa awali mbele ya wapelelezi na kudai walifanyiwa udhalimu mkubwa baad ya kuteswa..

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.