Pata taarifa kuu
USALAMA - DIPLOMASIA

Rais Afwerki amekanusha kuhusika katika mzozo wa Ethiopia

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki, siku ya Alhamisi, kwenye ziara ya siku mbili nchini kenya, amekanusha kuhusika kwa vyovyote kwenye mzozo wa Ethiopia.

Rais wa Eritrea Isaias Afwerki
Rais wa Eritrea Isaias Afwerki madote.com
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Afwerki amekanusha madai kuwa wanajeshi wa Eritrea walikiuka haki za binadamu katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, wakati wa vita vya miaka miwili, kadhalika alielezea kuendelea kuwepo kwa vikosi vya Eritrea nchini Ethiopia.

Sina nia ya kuingilia suala hili licha ya kampeni ya upotoshaji inayoendelea kujaribu kuvuruga mchakato wa amani nchini Ethiopia na kujaribu kuunda mzozo kati ya Eritrea na Ethiopia. Msichukulie Eritrea kama kisingizio cha matatizo ya Ethiopia au kwingineko katika eneo zima. Amesema kiongozi huyo wa Eritrea.

Vikosi vya Eritrea viliunga mkono vikosi vya Ethiopia wakati wa mapambano dhidi ya kundi la Tigray People's Liberation Front (TPLF), licha ya kuendelea kutuhumiwa na Marekani na mashirika ya haki za binadamu kwa kuhusika na baadhi ya ukatili mbaya zaidi wa mzozo huo.

Mapigano nchini Ethiopia yalikomeshwa kwa kusaini mkataba wa amani mwezi Novemba mwaka jana, ambao ulitaka kuondolewa kwa majeshi ya kigeni.

Matokeo ya mkataba

Tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo ya amani, shughuli ya kupeleka misaada katika eneo la Tigray imerejelewa, eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikabiliwa na uhaba wa chakula, madawa na hata mafuta.

Eneo la Tigray ambalo zaidi ya raia milioni sita wameathirika, huduma za kimsingi mfano mawasiliano, benki na umeme pia zinaendelea kurejeshwa polepole.

Wanachama wa taasisi iliyoundwa inayohusisha wanachama kutoka serikali ya Ethiopia na TPLF, watafanya mkutano wao wa kwanza Ijumaa hii, unaolenga kutathmini iwapo pande zote zinaheshimu mkataba.

Diplomasia yaimarishwa

Rais Afwerki baada ya kukutana na rais Ruto, wawili hao wametangaza  kuwa raia wa nchi hizo mbili wataingia nchi husika bila kuitishwa viza.

Tumekubali kukomesha hitaji la viza kabisa, kuanzia leo, na tumeagiza wizara zetu za mambo ya ndani  kufanyia kazi mbinu za kuidhinisha agizo hili. Wawili hao wamesema kwa taarifa ya pamoja.

Afwerki anazuru Kenya kwa ziara rasi kwa mara ya kwanza tangu Disemba 2018.

 

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.