Pata taarifa kuu

Mapigano makali yarindima mjini Tripoli, mji mkuu wa Libya

Raia mmoja ameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mapigano makali kati ya makundi yenye silaha katika mji mkuu wa Libya Tripoli, ambayo yamekuwa yakiendelea tangu Ijumaa usiku hadi Jumamosi, na kuzua hofu ya vita vipya.

Uharibifu uliyosababishwa na mashambulizi ya anga dhidi ya uwanja wa ndege Mitiga, mjini Tripoli, Libya, Mei 10, 2020.
Uharibifu uliyosababishwa na mashambulizi ya anga dhidi ya uwanja wa ndege Mitiga, mjini Tripoli, Libya, Mei 10, 2020. REUTERS/Ismail Zitouny
Matangazo ya kibiashara

Mapigano, kwa silaha nzito na nyepesi, yalizuka usiku katika vitongoji kadhaa vya Tripoli (magharibi), katikati mwa mgogoro wa kisiasa unaochochewa na serikali mbili zinazopingana.

Milio ya risasi na milipuko ya mabomu ilisikia usiku kucha na mapigano yameendelea Jumamosi saa sita mchana, kulingana na mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP.

Serikali yenye makao yake makuu mjini Tripoli imehusisha kambi ya serikali pinzani kwa mapigano hayo, hata kama "mazungumzo yanahitajika kufanyika ili kuepusha umwagaji damu katika mji mkuu", imesema katika taarifa.

"Tishio"

Vyombo vya habari nchini Libya vinaai kuwa raia pia wameuawa, lakini hakuna idadi rasmi iliyotolewa.

Hata hivyo shirika la habari la Libya, LANA, limetangaza kifo cha mwigizaji Mustapha Baraka ambaye alikuwa katika moja ya vitongoji katikati ya mapigano hayo. Kifo chake kiliamsha hisia kubwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo mara kwa mara alirusha video.

Mapigano hayo yalisababisha uharibifu mkubwa katikati mwa mji mkuu, kwa mujibu wa picha zilizorushwa kwenye mtandao, zikionyesha magari yaliyoteketea kwa moto na majengo yakiwa yameharibiwa kwa risasi. Msikiti na zahanati ya kibinafsi vimeteketea kwa moto, kulingana na picha hizi.

Serikali yenye makao yake makuu mjini Tripoli, inayoongozwa na Abdelhamid Dbeibah, imemshutumu mpinzani wake Waziri Mkuu Fathi Bachagha, ambaye yuko katikati mwa Sirte, kwa "kutekeleza vitisho vyake" vya kuutwaa mji huo.

Tangu kuteuliwa kwake mwezi Februari na Bunge lenye makao yake makuu Mashariki mwa nchi, Bw. Bachagha amekuwa akijaribu, bila mafanikio, kuingia Tripoli ili kuanzisha mamlaka yake, hivi karibuni akitishia kutumia nguvu kufanikisha hili. Hakujibu mara moja shutuma kutoka Tripoli.

Bwana Bachagha anaungwa mkono na mbabe wa kivita Khalifa Haftar, mwanajeshi mwenye ushawishi mkubwa mashariki mwa Libya, ambaye vikosi vyake vilijaribu kuuteka mji mkuu mwaka 2019.

Bw. Dbeibah, mkuu wa serikali ya mpito, anathibitisha kwamba atakabidhi madaraka kwa serikali iliyochaguliwa pekee.

Hofu yatanda

Mvutano kati ya makundi yenye silaha watiifu kwa kiongozi mmoja au kiongozi mwingine umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni mjini Tripoli. Mnamo Julai 22, mapigano yalisababisha vifo vya watu 16, ikiwa ni pamoja na raia, na karibu 50 kujeruhiwa.

"Marekani ina wasiwasi mkubwa kuhusu mapigano makali huko Tripoli," Ubalozi wa Marekani nchini Libya umesema.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya pia umesema "una wasiwasi mkubwa" na "mapigano (...) katika vitongoji vinavyokaliwa na raia, na kutaka "kusitishwa mara moja kwa uhasama".

Serikali iliyopo mjini Tripoli iliundwa mwanzoni mwa mwaka 2020 kutokana na mchakato uliofadhiliwa na Umoja wa Mataifa, ukiwa na dhamira kuu ya kuandaa uchaguzi mwezi wa Desemba mwaka jana lakini uliahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na tofauti kubwa katika misingi ya kisheria ya uchaguzi.

Libya ilitumbukia katika machafuko baada ya maandamano na mapigano yaliyosababisha kuanguka kwa utawala wa Muammar Gaddafi mwaka 2011. Katika miaka kumi na moja, nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika imeshuhudia serikali kadhaa, vita viwili vya wenyewe kwa wenyewe na haijawahi kuandaa uchaguzi wa urais.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.