Wafuasi wa watawala wa kijeshi Burkina Faso waandamana Ouagadougou
Nchini Burkina Faso, kumekuwa na maandamano ya raia kuunga mkono hatua ya jeshi kuchukua madarakani, huku Ufaransa na Umoja wa Mataifa ukilaani hatua hiyo.
Imechapishwa:
Wanajeshi waliochukua madaraka wanamzuia rais Roch Marc Christian Kabore, wanamshtumu kwa kushindwa kupambana na makundi ya kijihadi nchini humo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron,amesema analaani hatua hiyo ya mapinduzi na kuongeza kuwa, nchi yake inaunga mkono, msimamo wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, kulaani mapinduzi hayo.
Aidha, amesema amefahamishwa kuwa Kabore hayupo kwenye nafasi ya maisha yake kuhatarishwa, huku akisisitiza kuwa ukanda wa Afrika Magharibi kuendelea kushuhudia mapinduzi kunarudisha nyuma jitihada za kupambana na makundi ya kijihadi na ugaidi.
Naye, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kupitia msemaji wake Stéphane Dujarric ametaka kuachiwa kwa rais Kabore.
Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba aliyejitangaza kiongozi wa nchi hiyo, amesema nchi hiyo sasa iko chini ya vuguvugu jipya la kizalendo lililopewa jina la MPSR.