Nigeria: Zaidi ya wanafunzi 129 waliotekwa nyara waachiliwa
Makumi ya wanafunzi kutoka chuo cha Kiislamu magharibi mwa Nigeria, waliotekwa nyara karibu miezi mitatu iliyopita na sita kati yao waliofariki dunia wakiwa mikononi mwa watekaji nyara, wameachiliwa, mkuu wa shule hiyo ametangaza.
Imechapishwa:
Mnamo Mei 30, karibu watu 200 wenye silaha za kivita walivamia mji wa Tegina, Jimbo la Niger (magharibi mwa Nigeria), na kuwateka nyara wanafunzi 136 kutoka shule ya kibinafsi ya Waislamu Salihu Tanko.
Tangu mwezi Desemba, Nigeria imekumbwa na mfululizo wa visa vya utekaji nyara katika shule na vyuo vikuu.
Wanafunzi sita wa Tegina walifariki wakiwa mikononi mwa watekaji nyara na wengine kumi na tano waliweza kutoroka mnamo mwezi Juni, kulingana na uongozi wa shule.
"Wanafunzi wote wameachiliwa. Tunawapeleka nyumbani," mkuu wa shule ya Salihu Tanko, Abubakar Alhassan ameliambia shirika la habarila AFP. "Siwezi kutoa idadi kamili kwa sasa. Itabidi tuwaangalie mara tu tutakapofika nyumbani. Lakini hakuna mwanafunzi yeyote aliye mikononi mwa watekaji nyara."
Hakutoa maelezo kuhusiana na kuachiliwa kwa wanafunzi hao au kusema ikiwa walilipa fidia kabla ya kuachiliwa.
Maeneo ya Kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria yanakabiliwa na ongezeko la mashambulio, uporaji na utekaji nyara, vitendo vinavyoendeshwa na magenge ya wahalifu wanaojulikana kijijini kama "majambazi". Lakini mwaka huu, magenge hayo yalianza kulenga wanafunzi kwa kwa kutarajia fidia.