Raia wa Misri, Sudan na Ethiopia wasubiri matokeo ya mazungumzo Kinshasa
Mazungumzo ya siku tatu, kujaribu kutafuta mwafaka wa matumizi ya maji ya Mto Nile kufuatia hatua ya Ethiopia kujenga bwawa kubwa la kuzalisha umeme, yanamalizika leo jijini Kinshasa nchini DRC kati ya wawakilishi kutoka Ethiopia, Misri na Sudan.
Imechapishwa:
Misri inasema mazungmzo haya yanatoa nafasi ya mwisho kabla ya Ethiopia kuendelea kujaza bwawa lake kwa kutumia maji hayo, ili kufanikisha mradi wake ambao inasema utainufaisha kiuchumi, lakini Misri inasema mradi huo utawakosesha raia wake maji.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Thisekedi na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ndiye mpatanishi wa mazungumzo hayo.
Chanzo cha mgogoro
Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo limegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji yanayofika katika nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu.
Ethiopia nayo inasisitiza ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza bidhaa hiyo katika nchi za nje.