DRC yasema haitaki tena ushirikiano wa kijeshi na Ubelgiji
Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imetangaza kusitisha ushirikiano wake wa kijeshi na Ubelgiji.
Imechapishwa:
Taarifa zilizotolewa na Radio ya Umoja wa Mataifa ya Okapi, zimesema uamuzi wa serikali ya Kinshasa unakuja baada ya kushuhudia mvutano wa kisiasa wa chini kwa chini kati ya serikali hizo mbili tangu kuteuliwa kwa Waziri Mkuu mpya Bruno Tshibala.
Jarida la kila wiki la Jeune Afrique linalochapishwa nchini Ufaransa siku ya Alhamisi, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Ubelgiji Laurence Mortier, amesema amepokea taarifa hizo kutoka Kinshasa bila maelezo yoyote.
Aidha, amesema Brussels inaendelea kufanya tathmini ya ushirikiano huo na inataka ufafanuzi zaidi kuhusu hatua hii.
Ubelgiji imekuwa ikisaidia kijeshi nchi ya DRC kwa kuwapa mafunzo wanajeshi wake miongo kadhaa sasa kuwasaidia kupambana na makundi ya waasi.
Ushirikiano huo ulianza kutiwa dosari tangu kuanzishwa kwa Vita vya ukombozi vilivyofanikisha kuwepo utawala mpya chini ya Marehemu rais Laurent Desire Kabila, mwaka 1996 lakini uhusiano huu ukarejeshwa baada ya Joseph Kabila kuingia madarakani.