Pata taarifa kuu
DRC-KABILA

DRC: Rais Kabila aunga mkono makubaliano yaliyoratibiwa na maaskofu

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Joseph Kabila, amekubali na kuunga mkono makubaliano ya kisiasa yaliyoratibiwa na baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini humo, makubaliano yaliyolenga kumaliza sintofahamu ya kisiasa nchini humo. 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Joseph Kabila.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Joseph Kabila. REUTERS/Tiksa Negeri/File Photo
Matangazo ya kibiashara

Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki, usiku wa kuamkia mwaka mpya, walifanikiwa kuzishawishi pande zilizokuwa zinakinzana kisiasa nchini humo, kufikia makubaliano na kutia saini.

Makubaliano haya yanatoa nafasi ya kuundwa kwa baraza la kitaifa litakalosimamia utekelezwaji wa makubaliano haya, ambayo sasa yanamfanya rais Kabila kuendelea kusalia madarakani hadi mwishoni mwa mwaka huu.

"Mambo yako wazi kabisa baada ya mazungumzo kati ya rais na maaskofu, ambao amewataka kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana kutekeleza makubaliano hayo," alisema mmoja wa maaskofu waliohudhuria kikao hicho.

Mtu wa karibu na rais Kabila, amethibitisha kiongozi huyo kukutana na maaskofu hao lakini hakuweka wazi hasa kile ambacho rais Kabila aliwaambia maaskofu hao.

Rais Kabila ambaye amekuwa madarakani toka mwaka 2001, alitakiwa kuondoka madarakani Desemba 20 mwaka jana ambapo ndio muhula wake wa pili ulikuwa umefikia tamati, lakini aliendelea kusalia madarakani kufuatia makubaliano yaliyoratibiwa na umoja wa Afrika.

Jumanne ya wiki hii muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais Kabila, walisema kiongozi huyo anayo haki kuthibitisha makubaliano yaliyoratibiwa na maaskofu na kuonya kuwa vinginevyo huenda yakaiweka nchi hiyo pabaya.

Maaskofu hao wamewataka upande wa Serikali na upinzani kuwasilisha kwa maandishi, mapendekezo ya kuhusu namna ya kuteuliwa kwa waziri mkuu na ukubwa wa Serikali.

Hadi pale uchaguzi utakapofanyika mwishoni mwa mwaka huu, baraza maalumu la mpito litaundwa na kuongozwa na kiongozi mkongwe wa upinzani Etienne Tshisekedi na waziri mkuu atatoka pia kutoka upinzani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.