Pata taarifa kuu
RWANDA-HFCs

Rwanda: Nchi zaidi ya 200 duniani zakubaliana kuhusu kupunguza gesi ya HFCs

Zaidi ya nchi 150 zimefikia makubaliano ambayo wataalamu wanasema ni ya “kihistoria” katika juhudi za kuachana na matumizi ya gesi ambazo zinaleta madhara zaidi na kusababisha kuongezeka kwa hali ya joto duniani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) akiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame (kulia) jijini Kigali, October 15, 2016
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry (kushoto) akiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame (kulia) jijini Kigali, October 15, 2016 REUTERS/James Akena
Matangazo ya kibiashara

Wajumbe kutoka nchi mbalimbali duniani wamekubalian kupunguza matumizi ya gesi ya Hydroflurocarbons (HFCs), ambayo hutumiwa kwa kiasi kikubwa kwenye majokofu, viyoyozi na dawa za kutuliza harufu (air spray).

Wajumbe wanaohudhuria mkutano wa kimataifa jijini Kigali, Rwanda, wamekubaliana na kuidhinisha mapendekezo magumu ya Itifaki ya Montreal, makubaliano ambayo sasa yatashuhudia nchi tajiri zikipunguza zaidi matumizi ya gesi ya HFC kuanzia mwaka 2019.

Licha ya makubaliano haya wakosoaji wa mataifa yaliyoendelea na hasa yanayozalisha na kutumia gesi hii kwa wingi, wanasema kuwa huenda hatua zilizokubaliwa zisiwe na athari kwa kiasi kikubwa kama watu wengi walivyotarajia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry, ambaye alisaidia kufikiwa kwa makubaliano haya kwa kuwa na mikutano mfululizo kuwahakikishia wajumbe utayari wa nchi yake kuanza kupunguza matumizi ya gesi ya Hydroflurocarbons, alisema kuwa huu ni ushindi mkubwa kwa sayari ya dunia.

Wajumbe wa mkutano wa kimataifa wa kupunguza gesi ya HFCs wakiwa jijini Kigali, Rwanda, October 15, 2016
Wajumbe wa mkutano wa kimataifa wa kupunguza gesi ya HFCs wakiwa jijini Kigali, Rwanda, October 15, 2016 REUTERS/Cyril Ndegeya/Pool

Makubaliano haya yatashuhudia njia tatu zilichukuliwa na mataifa tofauti duniani, nchi tajiri kama zile za umoja wa Ulaya, Marekani na nyingine, zitaanza kudhibiti matumizi ya gesi ya HFCs katika kipindi cha miaka michache ijayo ambapo zitapunguza kwa karibu asilimia 10 kuanzia mwaka 2019.

Baadhi ya nchi zinazoendelea kama China na zile za Latin America na zile nchi za visiwa, zitaachana na matumizi ya gesi hiyo kuanzia mwaka 2024.

Nchi nyingine zinazoendelea, hasa India, Pakistan, Iran, Iraq na nchi za Ghuba zenyewe zitaanza kuchana na matumizi ya gesi hiyo kuanzia mwaka 2028.

Nchi ya China, ambayo ni mzalishaji mkubwa wa gesi ya HFCs haitapunguza uzalishaji wake au matumizi ya gesi hiyo mpaka mwaka 2029.

Kwa hakika, kama makubaliano haya yatatekelezwa kikamilifu yanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika mapambano ya dhidi ya hali ya joto duniani, ambapo wataalamu wanakadiria kuwa, utaondoa karibu tani bilioni 70 za hewa ya ukaa kutoka kwenye uso wa dunia ifikapo mwaka 2050.

Hata hivyo baadhi ya waangalizi wanahoji dhamira ya nchi ya China na India, wakitabiri kuwa zimefanya makubaliano haya kutokuwa na nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko na kwamba nia ya kupunguza hali ya joto duniani kwa nyuzi joto 0.5 inaweza isitimie.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.