Pata taarifa kuu
BURUNDI-EAC-USALAMA-SIASA

Yoweri Museveni aendelea na ziara yake Burundi

Msuluhishi mpya katika mgogoro wa Burundi, akiwa pia rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, anaendelea kukutana na wadau wote katika mzozo wa Burundi ili kujaribu kuutafutia suluhu.

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na Rais wa Uganda Yoweri Museveni mjini Bujumbura, Julai 14 mwaka 2015.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na Rais wa Uganda Yoweri Museveni mjini Bujumbura, Julai 14 mwaka 2015. RFI/Sonia Rolley
Matangazo ya kibiashara

Baada ya kukutana Jumanne jioni wiki hii na upinzani na vyama vya kiraia, Yoweri Museveni anatazamiwa leo mapema Jumatano asubuhi kukutana na wajumbe wa serikali, na baadae marais wa zamani. Yoweri Kaguta Museveni atahitimisha kazi yake hiyo kwa mkutano wa pamoja na wadau wote katika mzozo wa Burundi kwenye saa sita, saa za Afrika ya Kati.

Hata hivyo Upinzani umesema hauna matumaini kwa vikao hivyo kuwa vitazaa matunda yoyote, kwani, hasa kuwa rais Museveni hana uwezo wa kutafutia suluhu mzozo wa Burundi, ambapo chanzo cha mzozo huo ni muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza, wakati msuluhishi huyo mpya mwenyewe ana nia ya kuwania muhula mwengine katika uchaguzi wa urais, huku wapinzani nchini mwake wakiendelea kukandamizwa.

Rais Museveni alishiriki mara kadhaa katika mazungumzo ya kusaka amani nchini Burundi hadi kupatikana kwa Mkataba wa amani na maridhiano wa Arusha. Wakati huo rais Museveni alikua rais wa jitihada za kikanda kwa ajili ya mazungumzo ya Mkataba huo.

Rais Museveni aliteuliwa Julai 6 kama mpatanishi mpya katika mkutano wa kilele wa mwisho wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini Dar es Salaam, nchini Tanzania.

Upinzani ulilani na kutupilia mbali maazimio ya mkutano huo, ukitaja kwamba unamtetea rais Nkurunziza, lakini kambi ya rais ulikaribisha maazimio hayo.

Rais Yoweri Kaguta Museveni aliwasili mjini Bujumbura Jumanne mchana Julai 14 tofauti na asubuhi kama ilivyokua kwenye ratiba.

Uamzi wa kubadili ratiba hiyo ulichukuliwa na itifaki yake katika dakika za mwisho. Rais Yoweri Kaguta Museveni aliingia nchini Burundi kwa gari akipitia mkoani Kirundi Kaskazini mwa Burundi, kwenye mpaka na nchi ya Rwanda, na anatazamiwa kurejea leo Jumatano nchini mwake. Haijajulikana iwapo atarejea kwa gari au kwa ndege.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.