DRC: Serikali yanyoohewa kidole na waasi wa zamani wa M23
Ni mwaka mmoja sasa siku kwa siku tangu uasi wa zamani wa M23 utokomezwe kijeshi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tarehe 5 mwezi Novemba mwaka 2013.
Imechapishwa:
Jeshi la FARDC kwa kushirikia na Kikosi maalum cha Umoja wa mataifa nchini DRC (MONUSCO) limefanikiwa kutokomeza uasi huo ambapo idadi kubwa ya waasi hao wa zamani walikimbilia nchi jirani ya Rwanda na Uganda, nchi mbili ambazo zilituhumiwa na Umoja wa Mataifa kusaidia waasi hao.
Mchakato huo wa kuwasambaratisha waasi wa M23 umechukuliwa na serikali ya Kinshasa kama hatua muhimu kwa ajili ya amani mashariki mwa DRC ambapo kwa uhakika baadhi ya wachambuzi wanafikiri kuwa serikali kushindwa kutekeleza maazimio ya Nairobi ni kuwapa mwanya waasi hao kujipanga upya.
Sambamba na hayo, mashirika ya kiraia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanadai kwamba zipo harakati za chini kwa chini za kundi hilo kuundwa upya jambo ambalo linatupiliwa mbali na tume ya Umoja wa Mataifa nchini Congo Monusco, kwa vile hakuna ushahidi wa madai hayo.
Uenyekiti wa kundi hilo la M23 ulioko uhamishoni nchini Uganda, tayari umejibu tuhuma hizo kwa kusema kwamba uundwaji upya wa M23 si hoja ila hoja iliopo ni serikali kushindwa kutekeleza ahadi zake ambapo idadi ndogo tu ya waasi hao ndio waliopewa msamaha wa rais ikilinganishwa na ujumla wao.