Pata taarifa kuu
SOMALIA

Jeshi la Kenya laongoza mashambulizi dhidi ya Al Shabab nchini Somalia

Umoja wa Afrika unasema ndege za kijeshi za Kenya zimeshambulia ngome za kundi la kigaidi la Al Shabab nchini Somalia.

Wanamgambo wa Al Shabab nchini Somalia
Wanamgambo wa Al Shabab nchini Somalia
Matangazo ya kibiashara

Jeshi la AMISOM linasema mashambulizi hayo yamefanyika katika vijiji vya Anole na Kuday katika jimbo la Juba,  Kusini mwa nchi hiyo.

AMISOM, imekuwa ikiendelea na mashambulizi dhidi ya kundi hilo la kigaidi kwa lengo la kuliangamiza kabisa ndani ya nchi hiyo.

Msemaji wa kundi la Al Shabab, Abdulaziz Abu Musab amesema kuwa jeshi la Kenya na wale wa Umoja wa Afrika wameendelea kupambana na wapiganaji hao ardhini siku ya Jumatatu.

Makabiliano haya yanakuja juma moja baada ya kundi hilo kudai kuwa limetekeleza mauaji ya zaidi ya watu 60 katika eneo la Mpeketoni Pwani ya Kenya.

Al Shabab inasema imewaua wanajeshi kadhaa wa Kenya na miili yao imetapakaa katika vijiji hivyo wakati wa makabiliano hayo.

Baada ya kundi hilo kuondolewa mjini Mogadishu, limekuwa likiendelea na mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika.

Al Shabab wameendelea kutishia kuishambulia Kenya, Uganda, Djibouti na Ethiopia kwa sababu imetuma wanajeshi wake nchini humo.

Kenya na Uganda imetoa wito kwa raia wake kuwa makini kipindi hiki cha kombe la dunia kutokana na tishio kutoka kwa kundi hili la kigaidi.

Mwaka 2010, kipindi kama hiki jijini Kampala nchini Uganda watu zaidi ya 70 walipoteza maisha baada ya kushambuliwa na Al Shabab wakitizama michuano ya kombe la dunia.

Nchini Kenya, Wizara ya Usalama imetoa wito kwa wakenya kuepuka kutizama michuano ya soka katika maeneo ya umma na badala yake kusalia nyumbani.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.