Pata taarifa kuu
AU-SOMALIA

Jeshi la AMISOM kuongezewa nguvu ya kupambana na wapiganaji wa Al Shabaab nchini Somalia

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU wanaokutana jijini Addis Ababa nchini Ethiopia wameafikiana kuongeza idadi ya wanajeshi wanaopambana na wapiganaji wa kundi la Al-shabaab nchini Somalia, AMISOM.

Photo AFP / AU-UN IST PHOTO
Matangazo ya kibiashara

Baraza la amani na usalama la AU limesema AMISOM itaongezewa wanajeshi 6235 sawa na nyongeza ya asilimia 35 ili kuzidisha nguvu ya kulitokomeza kundi hilo lenye uhusiano na mtandao wa kigaidi duniani wa Al Qaeda.

Ongezeko hilo litafanya idadi ya wanajeshi wa AU waliopo nchini Somalia kufikia 23,996.

Hata hivyo pendekezo hilo ni lazima liidhinishwe na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UNSC kabla ya wanajeshi hao kupelekwa Somalia.

Pendekezo hilo linakuja majuma kadhaa baada ya kutekelezwa kwa shambulio la kigaidi nchini Kenya katika jengo la maduka la Westgate jijini Nairobi, tukio ambalo kundi la Al-shabaab lilikiri kuhusika nalo kwa madai ya kuishinikiza Kenya iondoe wanajeshi wake nchini humo.

Majeshi ya AMISOM yapo nchini Somalia toka mwaka 2007 na yanaundwa na wanajeshi kutoka Kenya, Uganda na Burundi.

Mkutano wa AU unaoendelea mpaka hii leo utashuhudia mjadala wa swala la nchi za Afrika kujitoa kwenye mahakama ya ICC kwa madai kuwa mahakama hiyo imekuwa haiwatendei haki viongozi wa Afrika.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anaelekeo Addis Ababa kuhudhuria mkutano huo na yeye na Naibu wake William Rutto ni miongoni mwa viongozi wa Afrika wanaokabiliwa na kesi katika mahakama hiyo.

Hata hivyo huenda kukashuhudiwa mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama wa AU kwani baadhi ya nchi zinaonyesha dalili ya kutokubaliana na hoja ya bara la Afrika kujiondoa katika mkataba wa Roma.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.