Pata taarifa kuu
BRAZIL 2014

Brazil na Uholanzi zapata ushindi kufika hatua ya 16 bora

Brazil itamenyana na Chile katika hatua ya mwondoano tarehe 28 mwezi huu katika michuano ya kombe la dunia, baada ya timu hizo mbili kufuzu katika hatua ya 16 bora Jumatatu usiku.

Neymar akishangilia bao
Neymar akishangilia bao REUTERS/Ivan Alvarado
Matangazo ya kibiashara

Uholanzi nao watamenyana na Mexico ambao pia walifuzu katika hatua hiyo muhimu ya mwondoano na watamenyana tarehe 29 mwezi huu wa Juni.

Wenyeji Brazil walimaliza katika nafasi ya kwanza katika kundi lao la A kwa alama 7 wakifuatwa na Mexico ambao pia wana alama 7.

Croatia na wawakilishi wa Afrika Cameroon wamebanduliwa nje ya michuano hiyo, huku Croatia wakimaliza wa tatu kwa alama tatu lakini Cameroon wanarudi nyumbani bila ya alama yoyote.

Katika mchuano wa kutamatisha kundi la A, Brazil walimaliza kwa ushindi mkubwa wa kupata mabao 4 kwa 1 dhidi ya Cameroon.

Neymar mshambulizi matata wa Brazil ambaye anaongoza katika safu ya ufungaji wa mabao katika michuano hii akiwa na mabao manne aliifungia timu yake mabao mawili katika mchuano wa Jumatatu.

Mshambulizi wa Brazil Neymar akidhibiti mpira dhidi ya mchezaji wa Cameroon Allan Nyom
Mshambulizi wa Brazil Neymar akidhibiti mpira dhidi ya mchezaji wa Cameroon Allan Nyom Reuters/David Gray

Mataifa ambayo tayari yamefuzu katika 16 bora:
Brazil (Kundi A)
Mexico ( Kundi A)
Netherlands (Kundi B)
Chile ( Kundi B)
Colombia (Kundi C)
Costa Rica (Kundi D)
Argentina (Kundi F)
Belgium (Kundi H)

Joel Matip aliipa Cameroon bao la kufuta machozi na bao la pekee la timu hiyo katika michuano hii.

Katika mchuano mwingine Jumatatu usiku, Mexico waliwafungisha virago Croatia kwa kuwafunga mabao 3 kwa 1 katika mchuano wa mwisho wa kundi hilo.

Bingwa mtetezi Uhispania ambayo tayari imebanduliwa katika michuano hii, ilipata ushindi wake wa pekee katika michuano hii kwa kupata ushindi wa mabao 3 kwa 0 dhidi ya Australia.

Mabao ya Uhispania yalitiwa kimyani na washambulizi David Villa, Fernando Torres na Juan Mata.

Ushindi wa Uhispani unamaanisha kuwa inamaliza ya tatu katika kundi lao B kwa alama 3, nyuma ya Chile ambao ina alama sita na Uholanzi ambayo inaogoza kundi hilo kwa alama 9 wakati Australia wakirudi nyumbani bila ya kupata ushindi wowote.

Uholanzi nao walimaliza kundi lao kwa kupata ushindi katika michuano yao yote na mabao ya Leroy Fer na Memphis Depay yaliwapa alama tatu vijana wa Kocha Loius Van Gaal.

Mshambulizi wa Uholanzi  Arjen Robben akishangilia bao
Mshambulizi wa Uholanzi Arjen Robben akishangilia bao REUTERS/Michaela Rehle

Mataifa yaliyobanduliwa nje ya michuano hii.
Cameroon ( Kundi A)
Croatia (Kundi A)
Australia ( Kundi B)
Spain ( Kundi B)
England (Kundi D)
Bosnia-Hercegovina (Kundi F)

Jumanne usiku, Costa Rica itamenyana na Uingereza, Italia na Uruguay.

Waafrika watakuwa wanaitazama Cote Dvoire kuona ikiwa watafuzu katika hatua ya 16 bora na usiku huu watamenyana na Ugiriki. Japan nayo itamenyana na Colombia.

Cote Dvoire inahitaji kuishinda Ugiriki au wakitoka sare Colombia iwashinde Japan.

Gervinho (Kushoto) na  Didier Drogba.
Gervinho (Kushoto) na Didier Drogba. REUTERS/Ruben Sprich

Colombia wanaongoza kundi la C kwa alama 6, Cote Dvoire ni wa pili kwa alama 3, Japan na Ugiriki wana alama 1.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.