Kyiv yadai kuchukua kijiji cha Staromayorske, kusini mwa Ukraine
Jeshi la Ukraine limechukua tena kutoka kwa vikosi vya Urusi kijiji cha Staromayorske, upande wa kusini, ambapo vikosi vya Kiev vimeongeza mashambulio yao katika siku za hivi karibuni, Naibu Waziri wa Ulinzi Ganna Maliar ametangaza.
Imechapishwa:
"Staromayorské katika eneo la Donetsk imekombolewa. Watetezi wetu kwa sasa wanafanya oparesheni za kuwaondoa wanajeshi wa Urusi, Naibu Waziri wa Ulinzi Ganna Maliar amesema kwenye Telegram.
Kulingana na maafisa wa nchi za Magharibi na Ukraine na hata wachambuzi, Ukraine imeanzisha mchakato wa kuyatimua majeshi ya Urusi kutoka kusini mashariki mwa nchi hiyo, kama sehemu ya mashambulizi yake ya wiki nzima ya kulipiza kisasi, ambapo wamepeleka maelfu ya majeshi katika eneo la mapambano.
Hayo yanajiri wakati rais Vladimir Putin wa Urusi amesema siku ya Alhamisi kuwa mapigano yamezidi mno katika eneo la Zaporizhzhia kusini mashariki mwa Ukraine.
Putin ambaye yuko mjini Saint Petersburg, amewapongeza wanajeshi wake kwa kile alichosema ni kuzuia mashambulizi ya Ukraine na kudai kwamba wamelitia hasara kubwa jeshi la Ukraine.
Mapigano makali yamekuwa yakiripotiwa katika wiki za hivi karibuni katika maeneo kadhaa huko Zaporizhzhia.