Pata taarifa kuu
HAKI-UFISADI

Bunge la Ulaya laondoa kinga ya wabunge wawili wanaolengwa na mahakama ya Ubelgiji

Wabunge waliokutana katika mji mkuu wa Umoja wa Ulaya, Brussels, wamepiga kura kwa kunyoosha mkono na kuidhinisha Mbelgiji Marc Tarabella na Muitaliano Andrea Cozzolino kuondolewa kinga, kama sehemu ya uchunguzi wa ufisadi ndani ya Bunge unaohusisha Qatar.

Bunge la Ulaya kabla ya kikao cha mashauriano mjini Brussels.
Bunge la Ulaya kabla ya kikao cha mashauriano mjini Brussels. REUTERS - POOL
Matangazo ya kibiashara

Mbelgiji Marc Tarabella na Muitaliano Andrea Cozzolino ambao wanashukiwa kupokea hongo ili kuendeleza maslahi ya Qatar na Morocco katika Bunge la Ulaya, waliotengwa kwa muda katika kundi la Socialists & Democrats (S&D), wanakanusha ubadhirifu wa aina yoyote.

Marc Tarabella, aliyepo kwenye makao makuu ya bunge la Umoja wa Ulaya, amepiga kura mwenyewe ya kumuondolea kinga.

'Nataka haki ifanye kazi yake'

Wabunge hao wawili waliochaguliwa, wataweza kusikilizwa na mahakama ya Ubelgiji. "Ni mbele ya haki kwamba nitatoa taarifa kuhusu maswali ambayo (wachunguzi) watataka kuniuliza. Nataka haki ifanye kazi yake,” amesema mbunge wa Ubelgiji alipoondoka. Eric Van Duyse, msemaji wa ofisi ya mwendesha mashitaka wa shirikisho la Ubelgiji, amebaini kwa upande wake kwamba kuanzia sasa na kuendelea "kila kitu kitawezekana, [...] hiyo haimaanishi kuwa kutakuwa na hatua za kulazimisha, lakini haki inatolewa kwa njia zote kuweza kufanya kazi kama mshitakiwa yeyote”.

Ripoti ya bunge juu ya kuondolewa kwa kinga yao, iliyoandikwa na mbunge wa Ufaransa Manon Aubry (LFI), inataja "zawadi za pesa" kupitia ushuhuda wa Mtaliano Pier Antonio Panzeri, mbunge wa zamani wa kisoshalisti aliyegeuka kuwa kiongozi wa shirika lisilo la kiserikali, ambaye alidai mnamo mwezi Desemba kuwa alilipa "kati ya euro 120,000 na 140,000", kwa awamu kadhaa, kwa Marc Tarabella kwa msaada wake katika masuala yanayohusiana na Qatar.

Makubaliano na mahakama

Pier Antonio Panzeri, aliyeshtakiwa na kuwekwa rumande kama washukiwa wengine watatu, alifikia makubaliano na mahakama mwezi Januari. Anajitolea kutoa taarifa juu ya mfumo wa rushwa ambao anakiri kushiriki, badala ya kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

(Pamoja na AFP)

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.