Pata taarifa kuu
URUSI-UINGEREZA-KOMBE LA DUNIA 2018

Urusi yasema mashabiki wa England watakuwa salama wakati wa kombe la dunia

Balozi wa Urusi nchini Uingereza amesisitiza kuwa mashabiki wa mpira wa timu ya taifa ya England watakuwa salama wakati wa mechi za fainali za kombe la dunia 2018 licha ya mzozo wa kidiplomasia baina ya nchi yao na utawala wa Moscow.

Balozi wa Urusi nchini Uingereza Alexander Yakovenko akizungumza jijini London, Machi 22, 2018
Balozi wa Urusi nchini Uingereza Alexander Yakovenko akizungumza jijini London, Machi 22, 2018 REUTERS/Simon Dawson
Matangazo ya kibiashara

“Watakuwa salama nchini Urusi,” amesema balozi Alexander Yakovenko wakati alipozungumza na wanahabari kwenye ofisi za ubalozi wake jijini London.

Balozi Yakovenko amesema hatua zote muhimu zimeshachukuliwa na mamlaka maalumu za Uingereza wanawasiliana na mamlaka husika za Urusi ili kutoa usalama kwa mashabiki hao.

“Ni hatua za kawaida tu ambazo tunachukua kama nchi nyingine yeyote ingeweza kufanya.”

“Nna uhakika kutakuwa na usalama wa kutosha, na kwa kuwakumbusha tu kutakuwa hakuna haja ya kulipa visa kwa wale watakaoingia Moscow.” amesema balozi Yakovenko.

“Mashabiki hawa watakuwa wageni wa Urusi.”

Matamshi yake yamekuja wakati huu kukishuhudiwa majibizano makali ya maneni kati ya Urusi na Uingereza kuhusu kupewa sumu kwa jasusi wa zamani wa Urusi kwenye ardhi ya Uingereza Machi 4, tukio ambalo Urusi imekanusha kuhusika.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson, Jumatano ya wiki hii aliitaka nchi ya Urusi kutoa hakikisho la usalama kwa mashabiki wa England wakati wa michezo ya kombe la dunia mwezi Juni na Julai.

Waziri Johnson pia amesema rais wa Urusi Vladimir Putin atatumia fainali za mwaka huu kujimarisha na kutafuta sifa kama alivyofanya mwenzake wa Ujerumani Adolf Hitler wakati wa michezo ya olimpiki mjini Berlin.

Johnson alikuwa akikubaliana na matamshi ya mbunge mmoja aliyedai kuwa rais Putin atatumia fainali za mwaka huu kueneza propganda yake kwa dunia kama alivyofanyab Hitler kwenye michezo ya olimpiki mwaka 1936.

Hata hivyo balozi Yakovenko amekashifu vikali matamshi ya Boris aliyesema hawezi kumfanisha kiongozi wao na Hitler.

“Nimeruhusiwa kusema kuwa Moscow inachukulia matamshi kama haya kama hayakubaliki na nikutowajibika kwa viongozi.” alisema balozi Yakovenko.

“Uingereza iko huru kufanya maamuzi yoyote kuhusu ushiriki wake kwenye fainali za mwaka huu lakini hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kuwatukana raia wa urusi ambao walipigana kuumaliza utawala wa Kinazi.”

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.