Miezi 7 yaongezwa katika mazungumzo kati ya Iran na nchi zenye nguvu
Nchi ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani yameshindwa kufikia muafaka katika siku ya mwisho Jumatatu Novemba 24 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Nchi hizo sita pamoja na Iran zimekubaliana kuongeza miezi mingine saba ya mazungumzo kati yao.
Kushindwa kufikiwa kwa makubaliano hayo siku ya Jumatatu, kumefuatia mazungumzo ya kina yaliyofanyika kwa zaidi ya siku tano mjini Vienna, Austria kati ya ujumbe wa Iran, Marekani, Urusi, China, Uingereza, Ufaransa pamoja na Ujerumani.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, John Kerry amesema kuwa licha ya kutofikiwa muafaka lakini walau wamepiga hatua kwenye mazungumzo yao.
Kauli ya waziri Kerry iliungwa mkono na waziri mwenzake wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Philip Hammond ambaye amesema licha ya kupiga hatua kwenye mazungumzo hayo changamoto bado ni kubwa.