Pata taarifa kuu
USWISI-DRC-VIKWAZO-SIASA

Uswisi yachukua vikwazo dhidi ya wasaidizi wa Kabila

Uswisi imechukua vikwazo dhidi ya maafisa 14 walio karibu na Rais Joseph Kabila wanaoshutumiwa kufanya makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu na kuzuia mchakato wa kidemokrasia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila. © AFP PHOTO/ALAIN WANDIMOYI
Matangazo ya kibiashara

Wanasiasa ni miongoni mwa watu hao vigogo waliochukuliwa vikwazo na Uswisi, ikiwa ni pamoja na Lambert Mende, Waziri wa Habari na msemaji wa serikali. Uswisi inamshtumu kuendesha sera ya uharibifu dhidi ya vyombo vya habari.

Ramazani Shadari na Evariste Boshab, mawaziri wawili wa zamani wa mambo ya ndani, pia wanakabiliwa na vikwazo hivyo. Wanashutumiwa kuchochea na kuandaa ukandamizaji dhidi ya upinzani.

Vikwazo hivi pia vinawalenga maafisa muhimu wa usalama. Maafisa hao ni pamoja na Kalev Mutond, Mkuuwa idara ya ujasusi nchini DRC. Uswisi inamshtumu kuwakamata kiholela wafuasi wa upinzani, lakini pia kuwafanyia vitisho.

Maafisa wa jeshi na polisi pia wanakabiliwa na hatua hiyo ya Uswisi.

Vikwazo hivi ni pamoja na kuzuiliwa kwa mali ya watu hawa nchini Uswisi pamoja na kupigwa marufuku ya kuingia au kusafiri nchini Uswis.

Kabla ya Uswisi, Umoja wa Ulaya na Marekani tayari wamechukua hatua kama hizi dhidi ya maafisa walio karibu na Rais Joseph Kabila.

Kabila, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 17 anaendelea kushinikizwa kutowania tena katika uchaguzi wa urais. Muhula wake ulimalizika tangu mwaka mmoja uliyopita. Lakini ameendelea kusalia madarakani, akidai kuwa katiba haiko wazi kuhusu suala hilo.

Katika miezi ya hivi karibuni, upinzani na Kanisa Katoliki walizidisha shinikizo zaidi kwa rais, ambaye annashtumiwa kutaka kusalia madarakani. Lakini maandamano dhidi ya serikali yake yamekua yakipigwa marufuku na kukandamizwa na polisi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.