Pata taarifa kuu
WAFCON 2024

Kenya na Botswana kumenyana kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kina dada 2024

Nyayo Stadium, Nairobi Kenya – Timu ya taifa ya soka ya kina dada ya Kenya Harambee Starlets na Botswana zimekamilisha mazoezi ya mwisho leo katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi nchini Kenya kabla ya kupambana hapo kesho, Jumatano, kwenye awamu ya mwisho mkondo wa kwanza kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika itakayoandaliwa mwaka ujao nchini Morocco.

Harambee Starlets kabla ya mazoezi uwanjani Nyayo jijini Nairobi, Kenya 28/11/2023
Harambee Starlets kabla ya mazoezi uwanjani Nyayo jijini Nairobi, Kenya 28/11/2023 © Football Kenya Federation
Matangazo ya kibiashara

Kenya ilifanya mazoezi asubuhi nayo Botswana ikakamilisha mazoezi mchana. Kenya itakosa huduma za mshambuliaji Jentrix Shikangwa kupitia jeraha na mshambuliaji Esse Akida ambaye alitemwa katika kikosi cha awali, lakini kiungo Sheryl Angachi amerejea kikosini baada ya kuhofiwa kukosa kucheza kufuatia mazoezi ya kijeshi na klabu yake ya Ulinzi Starlets. Mshambuliaji Teresa Engesha hakuwa mazoezini leo licha ya kufanya mazoezi jana.

Marjolene Nekesa anayechezea klabu ya Slavia Praha katika nchi ya Jamhuri ya Czech na nahodha wa zamani Dorcas Shikobe ni miongoni mwa wachezaji ambao walikosa mechi dhidi ya Cameroon mwezi Septemba.

Sheryl ni mchezaji mzuri na nafurahia sana yuko hapa nasi. Nashukuru sana wizara kwa juhudi zao kusaidia klabu yake kumruhusu kuja. Hatuna presha yoyote kuanza nyumbani, wasichana wako imara na tutajituma. Botswana si timu rahisi na si timu ngumu. Wamepiga hatua kutuliko lakini tuko mbioni pia.

Kiungo wa Kenya, Cynthia Shilwatso, mazoezini.
Kiungo wa Kenya, Cynthia Shilwatso, mazoezini. © Football Kenya Federation

Nahodha wa Kenya Ruth Ingotsi ameahidi ushindi kwa mashabiki naye mshambuliaji Mwanahalima Adam akitoa ujumbe kwa mashabiki kujaza uwanja ili kuwatia motisha.

“Hatutawaangusha. Mungu mbele, sisi nyuma. WAFCON tunaenda safari hii,” alisisitiza Mwanahalima Adam anayechezea klabu ya Hakkarigücü Spor nchini Uturuki.

Waziri wa michezo nchini Kenya, Ababu Namwamba ametoa ahadi ya dola elfu 32,657 (€29,829) ikiwa Starlets watafuzu mashindano hayo.

Kilicho kizuri kwa wavulana lazima pia kifanyike kwa wasichana wetu. Pia tuna mipango tayari ya kuipeleka Starlets katika nchi moja barani Ulaya kuweka kambi ya mazoezi baada ya kufuzu.

Waziri wa michezo nchini Kenya, Ababu Namwamba akimsalimu kiungo mshambuliaji Elizabeth Wambui na wachezaji wengine
Waziri wa michezo nchini Kenya, Ababu Namwamba akimsalimu kiungo mshambuliaji Elizabeth Wambui na wachezaji wengine © Football Kenya Federation

Kulingana na kocha wa Botswana Basimanebothle Alex Malete wachezaji wote wako katika hali nzuri. Hamna majeraha yoyote na kinajumuisha wachezaji kutoka timu ya taifa walio chini ya miaka ishirini.

 

Tunaelewa mechi ni ya mikondo miwili na itatubidi tukabiliane na mahitaji ya mchezo wa kesho jinsi Kenya itakavyobadilisha mbinu zake kiufundi, kufuatia kukosa wachezaji wawili mahiri wa kikosi cha kwanza.

Kocha Alex haogopi kucheza mbele ya mashabiki wa Kenya ambao mara nyingi hujitokeza kwa wingi kushabikia timu zao.

Mechi zetu nyingi za mtoano kwenye mashindano tumeanza ugenini - dhidi ya Gabon, Tanzania, Zambia - kwa hivyo unaona tumezoea hayo mazingira.

Timu ya taifa ya Botswana kabla ya mazoezi uwanjani Nyayo
Timu ya taifa ya Botswana kabla ya mazoezi uwanjani Nyayo © Football Kenya Federation

Botswana ilifuzu awamu hii ya mwisho baada ya kuishinda Gabon kwa jumla ya mabao 10-1 lakini kocha Alex anasema "mechi huwa tofauti, Gabon si Kenya na Cameroon si Botswana. Tutatumia mbinu tofauti kabisa kwenye huu mchezo tofauti na mechi zilizopita."

 

Kikosi hicho pia kilisafiri na kocha wa timu ya taifa ya wanaume Didier Gomes Da Rosa ambaye kocha Alex anasema inaongeza nguvu kikosini.

Ni kocha mzoefu na anajua mpira sana. Tunajivunia yuko hapa kutupa motisha kama timu na pia kama taifa.

Mwamuzi wa kati wa mchezo huu atakuwa Shahenda Saad Saad Ali Elmaghrabi akisaidiwa na Yara Atef na May Ali Mahmoud Hassan kutoka Misri. Noura Samir Hamed ndiye mwamuzi wa nne.

Mechi ya marudio itachezwa tarehe 5 Disemba nchini Botswana. Mshindi wa jumla atafuzu moja kwa moja Kombe la Mataifa ya Afrika ya kina dada mwaka ujao nchini Morocco.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.