Pata taarifa kuu
FIFA-BLAZER-BLATTER

Fifa yamfungia maisha kujihusisha na soka aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo, Chuck Blazer

Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA limetangaza kumfungia maisha kujihusisha na masuala ya soka kwa aliyekuwa katibu mkuu wa shirikisho la soka Amerika Kusini Concacaf na pia mjumbe wa kamati kuu ya Fifa, Chuck Blazer. 

Chuck Blazer (Kushoto), akiwa na rais wa Fifa Sepp Blatter (Kulia) walipokutana mjini Frankfurt, 13/06/2005
Chuck Blazer (Kushoto), akiwa na rais wa Fifa Sepp Blatter (Kulia) walipokutana mjini Frankfurt, 13/06/2005 REUTERS/Kai Pfaffenbach
Matangazo ya kibiashara

Blazer mwenye umri wa miaka 70 hivi sasa alifanya kazi kama jasusi kwa kushirikiana na mwendesha mashtaka wa Marekani baada ya kukiri kuhusika na vitendo vya rushwa, utakatishaji wa fedha na ukwepaji kodi.

Kwenye taarifa yake Fifa imesema kuwa Blazer amefanya makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kwenda kinyume na sheria za mpira zinazoongoza shirikisho hilo.

Mwezi may mwaka huu maofisa kadhaa wa shirikisho la mpira wa miguu duniani Fifa walikamatwa nchini Uswisi wakihusishwa na tuhuma mbalimbali za rushwa.

Blazer, kiongozi wa pili wa ngazi ya juu katika shirikisho la Fifa kwa nchi za Amerika Kusini na kati toka mwaka 1990 hadi mwaka 2011, alihudumu pia kama mjumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo toka mwaka 1997 hadi mwaka 2013.

Katika kesi yake ya masuala ya rushwa kwenye mahakama ya Marekani, Blazer alikiri makosa 10 ya rushwa, ukwepaji kodi na utakatishaji wa fedha akiwa kama kiongozi wa juu wa Fifa.

Kwenye ushahidi wake, Blazer aliwaambia maofisa wa upelelezi wa Marekani, kuwa yeye pamoja na wajumbe wengine wa kamati ya utendaji ya Fifa walikubali kupokea rushwa ya fedha inayohusishwa na mpango uliowezesha kuipatia zabuni nchi ya Afrika Kusini kuandaa michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2010.

Blazer alienda mbali zaidi na kuongeza kuwa vitendo hivyo havikuishia hapo kwani pia yeye pamoja na wengine walishiriki pia kupokea rushwa kwaajili ya kuandaa fainali za kombe la dunia za mwaka 1998.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo maofisa usalama wa Marekani wanazo, zinaonesha kuwa Blazer kwa siri kubwa alifanya kazi kama jasusi na maofisa wa upelelezi wa Marekani kurekodi vikao vya juu vya utendaji vya Fifa.

Fifa inasema kuwa hatua hii imechukuliwa baada ya kujiridhisha kuwa Blazer alikiuka kanuni na sheria za Fifa kwa kushirikiana na vyombo vya dola, kurekodi mawasiliano ya siri ya vikao vyakamati ya utendaji, na kwamba uchunguzi wao ulianza mwaka 2014.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.