Pata taarifa kuu
SOKA

Misri kumenyana na Zambia katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki

Shirikisho la soka nchini Misri limetangaza kuwa timu ya soka ya taifa itamenyana na Zambia katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki tarehe 14 mwezi Novemba jijini Cairo.

Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo ni muhimu kwa Misri ambayo inajiandaa kwa mchuano wa mzuguko wa pili na  wa mwisho wa kusaka tiketi ya kufuzu katika kombe la dunia mwaka ujao nchini Brazil.

Kocha wa Misri Bob Bradley amesema kuwa mchuano huo ni muhimu sana kwa vijana wake ambao walifungwa mabao 6 kwa 1 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza mjini Kumasi nchini Ghana baada ya timu za Ethiopia na Sudan kukataa kucheza na timu yake.

Mchuano huo wa kirafiki utachezwa katika uwanja wa kijeshi jijini Cairo baada ya jeshi nchini humo kuithibishia Zambia usalama wao.

Wakati uo huo, Shirikisho la soka duniani FIFA limeamua kuwa mchuano wa marudiano dhidi ya Ghana utachezwa jijini Cairo na hautahamishwa katika uwanja mwingine nje ya nchi hiyo kama ilivyopendekezwa na Ghana hapo awali.

FIFA imefafanua kuwa imeridhika na maandalizi ya usalama jijini Cairo na kuihakikishia Ghana kuwa jeshi litawalinda nje na ndani ya uwanja huo wakati wa mchuano huo wa Kimataifa.

Aidha, Shirikisho hilo la soka limesema kuwa uamuzi wao pia umetolewa baada ya klabu ya Al Ahly kuruhusiwa kucheza mchuano wake wa nyumbani wa kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika jijini Cairo.

Uamuzi wa FIFA unamaanisha kuwa mashabiki wataruhusiwa kushuhudia mchuano huo utakaochezwa tarehe 19 mwezi Novemba.

Chama cha soka nchini Ghana kiliiomba FIFA kuruhusu mchuano huo kuchezwa katika uwanja mwingine baada ya kuhofia visa vya ukosefu wa usalama kutokana na maandamano ambayo yamekuwa yakishuhudiwa nchini humo kwa sababu za kisiasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.