Pata taarifa kuu
SOKA

Andre na Jordan Ayew wakubali kuichezea Ghana

Wachezaji wa kimataifa wa mchezo wa soka Ghana Andre na Jordan Ayew hatimaye wamekubali kurejea nyumbani na kuichezea Blacks Stars baada ya awali kukataa kuichezea timu hiyo kwa madai kuwa walidhalalishwa.

Matangazo ya kibiashara

Kaka hao wawili wanaochezea klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa wameafikia hilo baada ya mazungumzo yao na rais John Mahama jiji Accra.

Wawili hao walijiondoa katika timu ya taifa baada ya kutofautiana na uongozi wa shirikisho la soka na kocha Kwesi Appiah wakati wa michuano ya kuwania taji la timu bora barani Afrika nchini Afrika Kusini mapema mwaka huu.

Jordan alimshutumu kocha Appiah kwa kutomjumuisha katika kikosi chake huku Andre naye akitofautiana na viongozi wa shirikisho la soka, tofauti ambazo wanasema zimesuluhishwa.

Rais Mahama alikutana mara ya kwanza na wachezaji hao nchini Ufaransa na sasa wamekubali kuichezea Black Stars kuisaidia kufuzu kwa kombe la dunia nchini Brazil mwaka ujao.

Hata hivyo, Andre na Jordan wamesema kuwa hawawezi kucheza soka kwa masharti na kusema kuwa hawakupewa masharti yeyote ya kurudi kuichezea Ghana.

Waziri wa michezo nchini humo Elvis Afriyie Ankrah amesema kuwa ilimbidi rais kuingilia kati suala hilo ili wachezaji hao waisaidie Black Stars kufuzu katika kombe la dunia kutokana na  ubora wao wa kucheza soka.

Wachezaji hao sasa watakuwa tayari kuichezea Ghana mwezi Septemba mwaka huu dhidi ya Zambia lakini inasuburiwa kuona ikiwa kocha Kwesi Appiah atawaita kwenye kikosi chake.

Ghana ni wa pili katika kundi lao kwa alama 9, kundi linaloongozwa na Zambia kwa alama 10.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.