Pata taarifa kuu
UINGEREZA

Manchester United na City waendelea kupambana kwenye mbio za Ubingwa nchini Uingereza

Klabu ya Manchester United ilifanikiwa kupunguza tofauti ya pointi na kusalia pointi tatu dhidi ya vinara Manchester City baada ya kufanikiwa kuifunga Arsenal kwenye Uwanja wake wa nyumbani Emirates kwa magoli 2-1.

Matangazo ya kibiashara

Manchester United ambayo ilionekana kutawala sehemu kubwa ya mchezo ilikuwa ya kwanza kupata goli kupitia kwa Antonio Valencia ambaye aliunganisha mpira wa Ryan Giggs na kuwafanya waongoze hadi mapumziko.

Kipindi cha Pili Arsenal walionekana kubadilisha mchezo wao na kufanikiwa kupata goli la kusawazisha kupitai mfungaji bora wa ligi hiyo Robin Van Persie ambaye aliunganisha pasi mwanana aliyopewa na kinda Oxlade-Chamberlain.

Manchester United wakapanda na hasira na hatimaye kupata goli la pili kupitia kwa Danny Welbeck ambaye aliweza kumalizia kazi nzuri ambayo ilifanywa na Valencia ambaye alionekana mwiba kwa Arsenal.

Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger aliwapandisha hasira mashabiki baada ya kumtoa Oxlade-Chamberlin na nafasi yake kuchukuliwa na Andrey Arshavin lakini mwenyewe amejitetea kwa kusema alifanya hivyo baada ya kuona kinda huyo amechoka.

Wenger pia amesema kuwa ameumizwa na kitendo cha timu yake kupoteza mchezo huo lakini amekiri ukomavu wa wachezaji wa Manchester United ndiyo ambao umewafanya wafungwe kwenye mchezo huo.

Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema kitendo cha wao kupata ushindi baada ya Manchester City kushinda kilikuwa ni muhimu sana kwenye harakati zao za kusaka ubingwa nchini Uingereza.

Kwenye mchezo wa awali Manchester City ilifanikiwa kupata pointi tatu muhimu mbele ya Tottenham baada ya kupata ushindi wa dakika za lala salama kwa magoli 3-2 na kuongeza pointi tatu juu.

Manchester City walilazimika kusubiri uamuzi wa Howard Webb wa kuwapa penalti katika dakika ya tisini na tatu na kisha Mario Balotteli akafanikiwa kufunga mkwaju huo na kuwapa ushindi muhimu kwao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.