Wanajeshi wa Israeli wameondoka katika hospitali ya Al-Shifa huko Gaza
Nairobi – Wanajeshi wa Israeli wameondoka kwenye eneo la Hospitali ya Al-Shifa, Kaskazini mwa Gaza, baada ya wiki mbili ya operesheni kuwasaka wapiganaji wa Hamas, walioshtumiwa kutumia hospitali hiyo kama kituo cha Makanda wake.
Imechapishwa:
Kabla ya kuondoka, Jeshi la Israeli limesema, limewauwa wapiganaji 200 wa Hamas kupitia operesheni yake ya ardhini na angani huku likiwakamata na kuwazuia washukiwa wengine zaidi ya 500 wa kundi hilo.
Aidha, limesema mbali na mauaji, limefanikiwa kunasa kiwango kikubwa cha silaha, vikiwemo vilipuzi pamoja na hela kutoka kwa Hamas.
Wizara ya afya kwenye ukanda wa Gaza, imesema licha ya kuondoka kwa wanajeshi wa Israeli, wameacha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu ya hospitali.
Wakati wa operesheni hiyo, wagonjwa kadhaa waliuawa na miili yao imekuwa ikizagaa huku miili mingine zaidi ya 20 ikipatikana baada ya kukayangwa na magari ya kijeshi ya Israeli kwa mujibu wa madaktari wa hospitali hiyo.
Baada ya hatua ya Israeli kuondoa vikosi vyake, kundi la Hamas linaitaka Mahakama ya Kimataifa ya ICC kuchunguza mauaji na visa vingine vya uhalifu vilivyofanyika kwenye hospitali ya Al Shifa huku wakiongeza kuwa wanaiwajibisha serikali ya Marekani na rais wake Joe Biden kwa mauaji yaliyotokea kwenye ukanda Gaza.