Pata taarifa kuu

Wanajeshi 36 wa Syria wauawa katika shambulizi la Israel karibu na Aleppo

Takriban wanajeshi 36 wa Syria waliuawa katika shambulizi la Israel lililolenga jimbo la Aleppo kaskazini mwa Syria alfajiri ya Ijumaa, Shirika la Haki za Binadamu la Syria (OSDH) limesema.

Jeshi la Syria katika jimbo la Allepo, Syria.
Jeshi la Syria katika jimbo la Allepo, Syria. AFP
Matangazo ya kibiashara

Kulingana na shirika la Haki za Binadamu la OSDH lenye makao yake makuu nchini Uingereza na ambalo lina mtandao mkubwa wa vyanzo nchini Syria, shambulio hili lilenga hasa "ghala za makombora za Hezbollah nchini Lebanon", ambayo inapigana upande wa serikali ya Syria.

"Takriban wanajeshi 36 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la Israel" ambalo lililenga eneo lililo karibu na uwanja wa ndege wa Aleppo, OSDH imesema.

Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya vifo kwa jeshi la Syria katika mashambulizi ya Israel tangu kuanza kwa vita huko Gaza karibu miezi sita iliyopita, kulingana na OSDH.

Kwa upande wake, chanzo cha kijeshi kilichonukuliwa na shirika  la serikali la Syria SANA kimeripoti "watu kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa miongoni mwa raia na wanajeshi" katika shambulio hilo.

"Adui ambaye ni Israel ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo tofauti huko Athriya, kusini mashariki mwa Aleppo," chanzo hicho kimesema.

Mashambulizi hayo pia yalilenga viwanda vilivyo chini ya Wizara ya Ulinzi ya Syria huko Safira karibu na Aleppo lakini kwa sasa viko chini ya udhibiti wa makundi yanayoiunga mkono Iran, kulingana na OSDH.

Likihojiwa na shirika la habari la AFP kutoka Jerusalem, jeshi la Israel limejibu "kutotoa maoni" kuhusu habari hizi za vyombo vya habari.

Jeshi la Israel limefanya mamia ya mashambulizi ya anga nchini Syria tangu kuanza kwa vita katika nchi hiyo jirani, hasa yakilenga makundi yanayoiunga mkono Iran.

Imezidisha mashambulizi yake tangu kuanza kwa vita huko Gaza mnamo mwezi wa Oktoba 2023 kati ya Israeli na Hamas ya Palestina.

Wakati huo huo, Israel na Hezbollah zimekuwa zikirushiana risasi kila siku kwenye mpaka wa Israel na Lebanon tangu kuanza kwa vita vya Gaza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.