Pata taarifa kuu

Iran yashambulia 'maeneo ya kundi la kigaidi' Kurdistan ya Iraq na Syria

Walinzi wa Mapinduzi ya Irani walitangaza mapema siku ya Jumanne kwamba walirusha makombora kadhaa ya balestiki kwenye maeneo ya "kigaidi" huko Iraq na Syria, na kuua angalau "raia wanne" huko Kurdistan ya Iraq kulingana na mamlaka za ndani katika eneo linalojitawala.

Moshi ukitokea kwa jengo lililoharibiwa huko Erbil baada ya shambulio la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran.
Moshi ukitokea kwa jengo lililoharibiwa huko Erbil baada ya shambulio la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran. © RUDAW TV via Reuters
Matangazo ya kibiashara

Takriban milipuko minne ilisikika pande zote za Erbil. Picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha moshi, wa makombora ya balestiki, karibu na Ubalozi mdogo wa Marekani, anaripoti mwandishi wetu huko Erbil, Marion Fontenille. Walinzi wa Mapinduzi ya Iran wamedai kulenga na kuharibu "makao makuu ya kijasusi" ambayo wamedai kuwa yalifanywa na Israeli, kama vile "muungano wa makundi ya kigaidi dhidi ya Iran" yalivyolengwa, kulingana na shirika la habari la IRNA.

Mamlaka za Kikurdi zinaripoti vifo vya takriban raia wanne. Miongoni mwa wahanga ni mfanyabiashara mashuhuri wa Kikurdi na familia yake nzima. Shughuli katika Uwanja wa ndege wa Erbil zimesitishwa. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Baraza la Usalama la Kurdistan linaishutumu Tehran kwa kutumia "madai yasiyo na msingi" kwa mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi ya eneo hilo. "Kilichotokea ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa eneo la Kurdistan na wa Iraq. Serikali ya shirikisho na jumuiya ya kimataifa haipaswi kukaa kimya mbele ya uhalifu huu,” imesema taarifa hiyo.

Kulingana na shirika la habari la IRNA, shambulio la Erbil linakuja kwa kulipiza kisasi mauaji ya hivi karibuni ya makamanda kadhaa wa Walinzi wa Mapinduzi, lakini pia ya viongozi wa "mhimili wa upinzani", jina lililopewa washirika wa Tehran katika vita vyake dhidi ya Israeli. Mnamo Januari 2, katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, shambulio linalohusishwa na Israeli liliua naibu kiongozi wa kundi la Hamas, Saleh al-Arouri, na maafisa wengine sita na watendaji wa kundi hili la wanamgamo wa Kiislamu kutoka Palestina. Katikati ya mwezi wa Januari, Wissam Tawil, afisa mkuu wa kijeshi wa Hezbollah ya Lebanon, aliuawa kusini mwa Lebanon na shambulio pia lililohusishwa na Israeli.

Nchini Syria, Jeshi la Walinzi limetangaza kwenye tovuti yake ya Sepah News kwamba "limetambua maeneo ya mikusanyiko ya makamanda na wapiganaji muhimu wanaohusishwa na operesheni za hivi karibuni za kigaidi, hasa kundi la Islamic State" na "limewaangamiza kwa kurusha idadi fulani ya makombora ya balestiki. Limebaini kwamba shambulio hili nchini Syria lilifanywa kwa "jibu la jinai za hivi karibuni za makundi ya kigaidi ambayo yamewauwa idadi fulani ya wapendwa wetu huko Kerman na Rask".

Mnamo Januari 3, washambuliaji walifanya shambulio la kujitoa mhanga dhidi ya umati uliokusanyika Kerman, kusini mwa Iran, wakati wa hafla ya ukumbusho karibu na kaburi la Jenerali Qassem Soleimani, kiongozi wa zamani wa operesheni za jeshi la Iran huko Mashariki ya Kati, aliyeuawa mnamo Januari 2020 na shambulio la Marekani nchini Iraq.

(Na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.