Pata taarifa kuu

Walinzi wa mpaka wa Saudi Arabia watuhumiwa kwa mauaji wa wahamiaji

Nairobi – Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch katika ripoti yake mpya, limewatuhumu walinzi wa mpaka wa Saudi kwa kutekeleza mauaji ya wahamiaji kwenye mpaka wa Yemen.

HRW iliitaka Riyadh kubadili sera yoyote ya kutumia nguvu dhidi ya wahamiaji na wanaotafuta hifadhi na kuutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza madai ya mauaji hayo
HRW iliitaka Riyadh kubadili sera yoyote ya kutumia nguvu dhidi ya wahamiaji na wanaotafuta hifadhi na kuutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza madai ya mauaji hayo © AFP
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Human Rights Watch, mamia ya watu, wengi wao wakiwa ni raia wa Ethiopia waliokuwa na lengo la kuvuka kutoka nchini  Yemen inayokumbwa na vita ili kufika Saudi Arabia, wameuawa kwa kupigwa risasi.

Shirika hilo limesema limewahoji wahamiaji 38 raia wa Ethiopia waliojaribu kuvuka kuingia nchini Saudi Arabia wakitokea nchini Yemen pamoja na kuchunguza picha za satellite, video na picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na taarifa kutoka kwa vyanzo vingine.

Baadhi ya walionusurika walieleza kushambuliwa kwa karibu huku walinzi wa mpakani wa Saudi wakiwauliza raia wa Ethiopia "wangependelea kupigwa risasi katika kiungo kipi cha miili yao", ripoti hiyo ilisema.

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 20 kutoka eneo la Oromia nchini Ethiopia alisema walinzi wa mpaka wa Saudi waliyatua  risasi kwenye kundi la wahamiaji waliokuwa wameachiwa kutoka kizuizini.

"Waliturushia risasi kama mvua. Ninapokumbuka, nalia," alisema.

"Nilimwona kijana mmoja akiomba msaada, akapoteza miguu yake yote miwili. Alikuwa akipiga kelele, alikuwa akisema, 'Unaniacha hapa? Tafadhali usiniache'. Hatukuweza kumsaidia kwa sababu tulikuwa tunakimbia kwa ajili ya kuokoa maisha yetu." alieleza zaidi.

HRW iliitaka Riyadh kubadili sera yoyote ya kutumia nguvu dhidi ya wahamiaji na wanaotafuta hifadhi na kuutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza madai ya mauaji hayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.